‎ Na Janeth Raphael -Michuzi TV-Dodoma 

‎Wizara ya Afya imezitaka hospitali nchini kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi huku ikiendelea kuwekeza katika sekta ya afya ili kukuza uchumi wa taifa. Hayo yamebainishwa jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kambi ya mafunzo na matibabu ya upasuaji wa koo, sikio na mfumo wa pua katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).

‎Katika hafla hiyo iliyofanyika Desemba 4, 2025, Mkurugenzi utawala na rasilimali watu kutoka Wizara ya afya,  Issa Jumanne Ng’imba amesema kuwa wizara imejipanga kufikia wananchi wote kupitia maboresho ya huduma za afya, amesema kuwa Hospitali ya BMH inapaswa kuendelea kutoa huduma bora bila kuchoka kwa manufaa ya nchi. Amesema kuwa kazi inayofanywa na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi, ni kubwa na inaonekana wazi katika namna hospitali inavyohudumia jamii.

‎Aidha, Ng’imba amebainisha kuwa ombi la vifaa na mafunzo ya madaktari wanne atalifikisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwa ajili ya kulifanyia kazi.

Ameongeza kuwa upasuaji wa masikio na koo ni eneo lililopewa kipaumbele na serikali kutokana na changamoto za vifo vinavyotokana na magonjwa hayo.

‎Katika hafla hiyo, serikali imekabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuimarisha huduma za dharura hospitalini hapo.

‎Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi amesema kuwa kambi hiyo imekuja sambamba na ugawaji wa magari ya wagonjwa. 

Aidha, amebainisha kuwa hospitali ina jumla ya wafanyakazi 1,090 huku kukiwa na upungufu wa wafanyakazi 300, ukiwemo upungufu wa wataalamu wa masikio ambapo wapo wanne dhidi ya uhitaji wa wataalamu wanane.

‎Aidha, Prof. Makubi amebainisha kuwa BMH inapokea wagonjwa 1,000 hadi 1,200 kwa siku, hivyo kuhitaji ongezeko la watumishi wa afya ili kutoa huduma kwa ufanisi. Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa kiwango kikubwa katika hospitali hiyo kupitia mafunzo na vifaa, hatua inayosaidia kuboresha huduma.

‎Ameeleza kuwa kambi hiyo ya upasuaji ilianza Desemba 1 na inatarajiwa kukamilika Desemba 7, 2025. Akizungumzia lengo la kambi hiyo, amesema kuwa inalenga kutoa matibabu kwa wananchi, ambapo watu 10 wenye changamoto za masikio wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji kati ya 30 waliyojitokeza. Aidha, amebainisha kuwa kwa siku hufanyika upasuaji wa mtu mmoja hadi wawili kutokana na muda na aina ya upasuaji.

‎Prof. Makubi amesema kuwa kambi hizo zitakuwa endelevu kwa wagonjwa watakaohitaji upasuaji, na upasuaji utaendelea kufanyika kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Pia, ametoa wito kwa wananchi wenye matatizo ya masikio kufika BMH na hospitali nyingine kwa ajili ya matibabu.

‎Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Hands-Giving Life (HGL)  Hatice Eller kutoka Uturuki amesema kuwa wamefurahishwa na nafasi ya kushirikiana na BMH kutokana na hospitali hiyo kuwa miongoni mwa hospitali bora nchini. Aidha, ameishukuru menejimenti ya BMH kwa ushirikiano mzuri tangu maandalizi hadi kuanza kwa huduma.

‎Mmoja wa madaktari Prof. Dr. Aysegiil Datiogly walioungana na msafara huo amesema kuwa mafunzo yatahusisha nadharia na vitendo ili kuwaongezea uwezo washiriki. 

Aidha, amebainisha kuwa matibabu yatatolewa zaidi kwa wagonjwa wenye changamoto za masikio, ingawa wengine pia watapata huduma kulingana na uhitaji.

‎Kambi hiyo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kupunguza mzigo wa wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa masikio, pua na koo ndani ya mkoa wa Dodoma.









 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...