Farida Mangube, Morogoro

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki umekabidhi msaada wa chakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi milioni 3.2 kwa Kituo cha Kulelea Watoto Amani kilichopo Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uwajibikaji wake kwa jamii.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Mohamed Adam Bori, alisema TFS inaendelea kutekeleza majukumu yake ya uhifadhi wa rasilimali za misitu sambamba na kusaidia jamii zinazozunguka maeneo yake ya kazi.

Alisema msaada huo unajumuisha bidhaa muhimu za matumizi ya kila siku zikiwemo sabuni, mafuta ya kupikia, mchele na unga, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 3.2.

“TFS si taasisi ya uhifadhi pekee, bali ni mdau wa maendeleo ya jamii. Tunatambua umuhimu wa kurejesha kwa jamii kama sehemu ya wajibu wetu wa kijamii,” alisema Bori.

Aidha, aliwahimiza taasisi nyingine na wadau wa maendeleo kuiga mfano huo kwa kusaidia makundi yenye uhitaji mkubwa, hususan watoto wenye changamoto za kiafya na kijamii.

Kwa upande wake, mlezi wa Kituo cha Kulelea Watoto Amani, Sister Mather Kimaro, alisema bado kuna changamoto kubwa ya jamii kutowakubali watoto wenye changamoto za akili na ulemavu wa viungo, hali inayosababisha baadhi yao kutelekezwa.

“Watoto wenye changamoto za akili na viungo bado hawana sauti ya kuwatetea kama ilivyo kwa makundi mengine, jambo linaloifanya kituo chetu kubeba jukumu kubwa la kuwahudumia,” alisema.

Aliongeza kuwa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto za kiuchumi ikiwemo uhaba wa chakula, magodoro na dawa, hususan kwa watoto wanaosumbuliwa na tatizo la kuanguka na kukakamaa, wanaohitaji dawa za mara kwa mara.

Kwa sasa, kituo hicho kinahudumia watoto 43, huku kikiendelea kuhitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuboresha huduma na ustawi wa watoto hao.

Naye mmoja wa watoto wa kituo hicho, Simon Ernesto, aliishukuru TFS kwa msaada huo akisema umeleta faraja na matumaini kwa watoto na walezi wa kituo cha Amani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...