*Na MASHAKA MHANDO, Tanga

WAKIMBIAJI wapatao 200, wengi wao wakiwa ni vijana, wanatarajiwa *kufukuza upepo* katika uzinduzi wa msimu wa kwanza wa 'Msomera Historical Marathon' utakaofanyika Desemba 13 mwaka huu katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Mbio hizo zimeanzishwa na Kampuni ya Mawasiliano na Uendelezaji Utamaduni nchini (yenye makao makuu Butiama, Mara) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni.

 **Kuunga Mkono Uamuzi wa Uhamaji**

Mratibu wa shindano hilo, Mashaka Mgeta, alisema mbio hizo zinakwenda kuwakutanisha vijana na wanariadha wakubwa kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kuunga mkono dhamira ya wananchi waliokuwa wakiishi wilayani Ngorongoro, Arusha, kuhamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera na kufanya makazi yao ya kudumu.

Mgeta, ambaye kitaaluma ni Mwandishi wa Habari na anahudumu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kama Ofisa Habari wa Mkoa, alisema kitendo cha kuacha eneo la Ngorongoro kuendelea kuhifadhiwa na kuendeleza utalii ni suala linalopaswa kuungwa mkono na kupongezwa.

"Kwetu sisi, baada ya kubaini nia yao nzuri ya kuhama kupisha uhifadhi na utalii kule Ngorongoro, tumeanzisha mbio hizi maalum kwa ajili ya kufanya *utetezi na kuelimisha* hasa makundi ya vijana wetu ili waweze kutambua fursa zinazoweza kupatikana kupitia uhifadhi na utalii," alisema Mgeta.

Aliongeza kuwa vijana lazima watambue fursa zinazopatikana katika maeneo mbalimbali kupitia sekta hizo na hivyo kuwa na jukumu la msingi la *kulinda na kuhifadhi* rasilimali za Taifa.

 *Amani na Fursa Katika Riadha*

Mgeta alisisitiza kuwa mbio hizo zinakwenda kufungua mnyororo wa mahusiano na dhamira ya wananchi kutambua na kuacha kwa hiari yao maeneo ya uhifadhi kwa faida ya utalii na uendelezaji wa rasilimali za Taifa.

"Tunataka vijana wajue, pasipokuwa na **amani na utulivu** katika Taifa letu, hatuwezi kunufaika na fursa hizi zilizopo. Mbio hizi zimebeba ujumbe na agenda ya **kudumisha Amani** ili fursa zilizopo nchini ziweze kuwanufaisha vijana katika nyanja mbalimbali," alifafanua.


*Kanuni na Taratibu za Riadha*

Akizungumzia utekelezaji, Katibu wa Chama Cha Riadha Mkoani Tanga (RT), *Ibrahim Adam*, alisema wazo hilo liliungwa mkono na watasimamia mbio hizo kufanyika kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria zinazotawala mchezo wa Riadha duniani.

Alithibitisha kuwa kutakuwa na *mbio ndefu (kilomita 42.2)*, *nusu Marathon (kilomita 21)*, *kilomita 10* na zile za **kujifurahisha (kilomita 5)**.

Adam alisema tayari njia zitakazopitwa na wakimbiaji zimefanyiwa ukaguzi, ikiwemo kujiridhisha na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vituo vya maji na *juice*, ili kuhakikisha wakimbiaji wanatengeneza wasifu wao huku wakifurahia maeneo ya kihistoria watakayopita wilayani Handeni hadi kufika Kijiji cha Msomera.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...