Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Temeke umebaini vitendo vya udanganyifu katika baadhi ya mabucha yanayouza nyama, baada ya kufanya operesheni maalum ya ukaguzi wa mizani inayotumika kuuzia wananchi.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Elolymus Hilary Maunde, amesema operesheni hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika maeneo ya Temeke na Kigamboni, ikiwa na lengo la kumlinda mlaji dhidi ya udanganyifu unaoweza kumsababishia hasara ya kifedha.

Amesema ukaguzi huo umefanyika katika kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu ambapo mahitaji ya vitoweo, hususan nyama, huongezeka kwa kasi, hali inayoweza kuwafanya baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kutumia mianya kujinufaisha.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, jumla ya mabucha 17 yalikaguliwa katika operesheni hiyo, ambapo mabucha matatu yalibainika kuchezea mizani kwa makusudi ili kuwaibia wananchi. Wamiliki wa mabucha hayo walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini kwa mujibu wa sheria.

Bwana Maunde amewataka wamiliki wa mabucha kuhakikisha wanasimamia kwa karibu shughuli za wafanyakazi wao na kutumia mizani iliyothibitishwa na Wakala wa Vipimo, ili kuepuka adhabu na kulinda uaminifu wa wateja wao.

Aidha, amewahimiza wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa zinazopimwa kwa mizani, na kutoa taarifa mapema kwa Wakala wa Vipimo endapo watabaini viashiria vya udanganyifu. Ofisi za Wakala huo zinapatikana katika kila mkoa na wilaya nchini kwa ajili ya kupokea malalamiko na kutoa msaada.

Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki katika zoezi hilo, akiwemo Jumamosi Kenneth Matanira na Joni Nzenze, wameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kufanya operesheni hiyo pamoja na kutoa elimu kwa wauzaji, wakisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uaminifu kati ya wauzaji na wateja pamoja na kuboresha biashara zao.

Operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha haki ya mlaji inalindwa na kwamba wananchi wanapata bidhaa kulingana na thamani halisi ya fedha wanazolipa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...