Watu wanne wamekamatwa na madini ya vito katika mtaa wa Togo, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, kufuatia operesheni maalum iliyofanywa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Ulanga na uongozi wa Wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema jana kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Afisa Madini Mkazi – Mahenge, Jonas Mwano, alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya taarifa za intelijensia kuonyesha uwepo wa biashara ya madini inayofanyika kinyume cha sheria katika makazi ya watu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema jana kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Afisa Madini Mkazi – Mahenge, Jonas Mwano, alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya taarifa za intelijensia kuonyesha uwepo wa biashara ya madini inayofanyika kinyume cha sheria katika makazi ya watu. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinalindwa na kunufaisha taifa kupitia mfumo rasmi wa masoko.
Watuhumiwa hao walikamatwa na madini mbalimbali yakiwemo Spinel, Rhodolite, Tourmaline na Volcanic Glass.
Madini hayo yalipatikana nyumbani kwa mmoja wao ambaye pia alikutwa akifanya usanifu wa madini bila kuwa na Leseni ya Usanifu wa Madini kinyume cha Sheria ya Madini Sura 123.
Alisema baada ya kukamatwa, watuhumiwa walifikishwa katika Kituo cha Polisi Mahenge na kufunguliwa jalada la uchunguzi MHE/IR/1189/2025, huku madini yote yakifanyiwa uthamini kubaini uzito, aina, ubora na thamani yake.
Aliendelea kusema kuwa tathmini inaonyesha kuwa madini hayo yana thamani ya Shilingi milioni 54.02, huku Serikali ikitarajia kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 5.05 kupitia kodi na tozo kutokana na madini hayo.
Mwano alisisitiza kuwa shughuli za usanifu wa madini zinaruhusiwa tu kwa mtu mwenye Leseni ya Usanifu wa Madini ambayo hulipiwa Shilingi za Kitanzania 2,930,256 sawa na Dola za Marekani 1,200 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa kukiuka matakwa hayo ni kwenda kinyume cha sheria na hatapewa nafasi mfanyabiashara yeyote anayejihusisha na shughuli hizo bila vibali.
Katika maagizo yake kwa wafanyabiashara wa madini, Mwano aliwataka kufanya biashara zao ndani ya Soko la Madini Mahenge, kuhakikisha wanakuwa na leseni halali na kuacha tabia ya kufanyia biashara majumbani au maeneo yasiyo rasmi.
Aidha, alisisitiza kuwa vitendo vya utoroshaji wa madini haviwezi kuvumiliwa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...