Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima , amewataka wanawake katika vikundi mbalimbali kueleza changamoto walizokumbana nazo katika mchakato wa kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi.

‎ Dkt. Gwajima ametoa wito huo Desemba 17, 2025 katika Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kutembelea na kufuatilia utekelezaji wa programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi.

‎Katika ziara hiyo, Waziri Gwajima ametembelea vikundi vya wanawake wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

‎‎Aidha, amefanya kikao na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi la wilaya hiyo, ambapo amebaini kuwa baadhi ya wanawake wanakumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa ujuzi wa kuandaa maandiko ya miradi, kushindwa kutimiza baadhi ya vigezo kama vile kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pamoja na changamoto nyingine zinazowafanya washindwe kunufaika na mikopo hiyo.

‎Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali, imeweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wanawake kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika upatikanaji wa mikopo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa miradi, kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi.

‎Amesisitiza kwamba, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kupitia programu za uwezeshaji kiuchumi.

‎ Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, ufuatiliaji wa karibu wa vikundi na majukwaa ya wanawake utasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu mahitaji halisi ya wanawake na kuboresha mifumo ya utoaji wa mikopo ili iwe rafiki, jumuishi na inayowafikia wanawake wengi zaidi.

‎‎Naye Diwani wa Kata ya Mbezi, Mhe. Pius Nyantoli, amesema kuwa kupitia uongozi wake ataendelea kufuatilia changamoto zinazowakabili wanawake katika eneo lake, ili kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha wanawake wanapata fursa stahiki za mikopo na kunufaika na programu za uwezeshaji kiuchumi.

‎Nao Wanawake wa Jukwaa walioshiriki katika kikao hicho wamemshukuru na kummpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na programu ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ambayo, inawapa fursa ya kujifunza jinsi ya kufikia uwezeshaji kiuchumi na kusema bayana changamoto zao.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...