Zaidi ya Shilingi milioni mia moja na mchango wa vifaa vya ujenzi, ikiwemo saruji zimepatikana katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa ofisi mpya ya kisasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tunduru, mradi unaotarajiwa kugharimu Shilingi milioni 200.

Harambee hiyo imewaleta pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo, wanachama na viongozi wa chama, ikiwa ni jitihada za pamoja za kuboresha miundombinu ya chama na kuimarisha mazingira ya utendaji katika ngazi ya wilaya.

Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, amesema Serikali inatambua na kutoa baraka za kiserikali kwa harambee hiyo, akieleza kuwa ni sehemu ya uzalendo na mchango wa wananchi katika kujenga misingi imara ya taasisi za kisiasa na kijamii.

Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa Serikali haina pingamizi lolote mradi harambee hiyo izingatie taratibu zilizopo, huku akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi na wadau wa maendeleo ni nyenzo muhimu katika kufanikisha miradi ya maendeleo wilayani humo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amekemea vikali tabia za baadhi ya watu na viongozi wanaojaribu kufubaza jitihada hizo za kizalendo, akisema vitendo hivyo vinachochewa na maslahi binafsi na siasa chafu zisizolenga maendeleo ya Wilaya ya Tunduru na wananchi wake.

Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhandisi Fadhili Chilombe, amesema uamuzi wa kujenga ofisi mpya umetokana na hali ya uchakavu wa ofisi ya zamani ya CCM, iliyojengwa mwaka 1965 na kuzinduliwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo kwa sasa ina zaidi ya miaka 60 na haikidhi mahitaji ya kiutendaji ya chama.

Akisisitiza hoja ya maendeleo, Mkuu wa Wilaya amesema Tunduru ni miongoni mwa wilaya kongwe nchini Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 1905, lakini maendeleo yake hayajaendana na historia na kongwe wa wilaya hiyo. Amesema hali hiyo inapaswa kuwa chachu kwa wananchi wa Tunduru kuungana, kuweka tofauti zao pembeni na kuunga mkono jitihada za kizalendo, ikiwemo ujenzi wa ofisi ya kisasa ya CCM, ili kuibadilisha wilaya hiyo na kuisukuma mbele kimaendeleo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mtila, amesema ujenzi wa ofisi mpya utaimarisha mazingira ya kazi, kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya chama na kuimarisha mshikamano wa wanachama, huku akitoa wito kwa wadau zaidi kujitokeza kuchangia ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...