Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt. Tumaini Msowoya, amewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Iringa kuwa makini na maisha ya chuoni kwa kujiepusha na ndoa za rejareja, makundi yasiyo na tija pamoja na tabia zinazoweza kuwavuruga kimasomo, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo na nidhamu binafsi.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuwapokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza, Dkt. Msowoya alisema licha ya wanafunzi kuwa na umri wa zaidi ya miaka 18 kisheria, bado wanapaswa kujiuliza iwapo ndoa au mahusiano ya kuishi pamoja ndiyo yamewaleta chuoni, au ni dhamira ya kutimiza ndoto zao za kielimu.
“Najua mna umri wa zaidi ya miaka 18 hivyo si watoto kwa mujibu wa sheria, lakini jiulizeni: je, ndoa ndiyo imekuleta chuoni? Wazazi wenu wanajua mmeoa au mmeolewa mkiwa hapa?” alihoji Dkt. Msowoya.
Aliongeza kuwa tafiti alizowahi kufanya kuhusu maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu zimebaini kuwa wanafunzi wengi huishi na wenza wao kwa siri bila familia zao kufahamu, jambo alilolitaja kuwa ni hatari na linaloweza kuathiri mwenendo wa masomo na maisha ya baadaye.
Dkt. Msowoya aliwahimiza wanafunzi kuipenda nchi yao, kusoma kwa bidii na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyo na mwelekeo chanya, akisisitiza kuwa wasomi ndio tegemeo la maendeleo ya taifa.
Katika hafla hiyo, Dkt. Msowoya alimwakilisha Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa ambaye alikuwa mgeni rasmi. Mwipopo aliwapongeza wanafunzi hao na kuchangia shilingi milioni 2,000,000 kwa ajili ya kuwasaidia katika safari yao ya masomo.
Amesisitiza kuwa nidhamu, maamuzi sahihi na uzalendo ni misingi muhimu kwa mwanafunzi yeyote anayelenga kufanikiwa chuoni na katika maisha kwa ujumla.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...