Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amezindua rasmi Kitita cha Huduma Muhimu ya Bima ya Afya kwa Wote, kinachotarajiwa kuanza kutumika Januari 26 mwaka huu, sambamba na kuanza kwa usajili wa wananchi awamu ya kwanza katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.Akizungumza leo Januari 24 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kilichowakutanisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara pamoja na watumishi walio chini ya Wizara hiyo, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mpango huo.
Mchengerwa amesema kitita hicho kitagharimu shilingi 150,000 kwa familia yenye watu wasiozidi sita, Ameeleza kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utazingatia wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao watagharamiwa na Serikali.
Waziri Mchengerwa amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura ya 161, Kifungu cha 13, imeanzisha kitita cha mafao ya huduma muhimu, na kwamba Kanuni ya 31(4) ya Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote (T.S. Na. 809 za mwaka 2024) zinampa Waziri wa Afya mamlaka ya kutangaza kwa umma kitita hicho.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, kitita cha huduma muhimu kwa awamu ya kwanza kitawahusisha mchangiaji, mwenza wa mchangiaji na wategemezi wanne ambao ni mzazi wa mwanachama au wa mwenza wake, mtoto wa kumzaa, kuasili au wa kambo, pamoja na ndugu wa mwanachama aliye chini ya umri wa miaka 21.
Kwa upande wake, Mratibu wa Bima ya Afya kwa wote Kitaifa, Tumainieli Macha, amesema dhana ya Bima ya Afya kwa Wote inalenga malipo ya kabla ya huduma, uchangiaji wa pamoja, uwajibikaji wa pamoja, usawa, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.
Ameongeza kuwa jumla ya wananchi 3,695,465, sawa na kaya 931,693, wametambuliwa kuwa ni wasio na uwezo, wakiwemo wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu. Aidha, wapo wazee 229 na watoto 267 wanaohudumiwa katika vituo maalum chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Amesema Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, jumla ya wananchi 1,457,602, sawa na kaya 276,004, wakiwemo wazee 229 na watoto 267, watasajiliwa na kugharamiwa na Serikali kupitia Halmashauri zote nchini.
Kwa ujumla, uzinduzi wa Kitita cha Huduma Muhimu ya Bima ya Afya kwa Wote unaashiria hatua muhimu ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakuwa endelevu, jumuishi na wenye tija kwa maendeleo ya afya ya jamii na taifa kwa ujumla.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...