Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa suala la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini limeendelea kuwa kipaumbele,ambapo Wizara hiyo imefanya marekebisho ya kanuni ya Ushirikishwaji wa wazawa ya mwaka 2018 ambapo Tume ya Madini itatangaza kupitia kanuni ya 13A orodha ya bidhaa na huduma ambazo zinatakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania zinazomilikiwa kwa asilimia 100.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Na kuongeza kuwa malengo ya kufanya hivyo ni kuingeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa manufaa mapana ya Taifa ambapo kwa awamu ya kwanza Novemba 14,2025 Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni hizo.
"Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018 ambapo Tume ya Madini mara kwa mara itatangaza kupitia Kanuni ya 13A orodha ya bidhaa na huduma ambazo zinatakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania ambazo zinamilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania, lengo likiwa ni kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa manufaa mapana ya taifa".
" Kwa awamu ya kwanza tarehe 14 Novemba, 2025 Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na kampuni za kitanzania kwa asilimia 100".
Aidha Waziri amesema kuwa katika kuendeleza suala hilo Tume ya Madini imeanzisha utaratibu wa kuendesha Majukwaa ya Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta hiyo kwa kila mwaka ambayo yanahusisha Wamiliki wa leseni, watoa huduma na wasambazaji bidhaa migodini,Taasisi mbalimbali za Serikali na Wizara na Taasisi zake lengo ikiwa ni kutathmini utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania.
" katika kufanikisha lengo la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za uchumi. Tume ya Madini imeanzisha utaratibu wa kuendesha Majukwaa ya Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini kila mwaka ambayo yanahusisha Wamiliki wa leseni, watoa huduma na wasambazaji bidhaa migodini, Taasisi mbalimbali za Serikali, Wizara ya Madini na Taasisi zake, Lengo la majukwaa hayo ni kutathmini utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania, kujadili changamoto zinazojitokeza na kuweka maazimio ya nini cha kufanya ili kuboresha ambapo hadi sasa Tume ya Madini imeshaendesha majukwaa manne ya ushirikishwaji wa watanzania kwa mafanikio makubwa.
Pia amesema katika miradi ya madini wameshuhudia ongezeko la ajira kwa Watanzania kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 ikiwa ni sawa na asilimia 95 kwa mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024.
Na katika nafasi zinazohitaji kupata uzoefu kutokana na kukua kwa teknolojia duniani, kumekuwa na utaratibu wa Kisheria wa urithishwaji wa Watanzania kwa nafasi zinazoshikiliwa na Wataalamu wa Kigeni ikiwa ni kutimiza azma ya Serikali ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaoshikilia nafasi za uongozi katika Kampuni za uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini.
Pamoja na hayo Waziri Mavunde ametumia Wasaa huo kutoa Rai kwa Watanzania kuendelea kuhakikisha wanapata utaalamu sahihi unaohitajika katika shughuli za madini ili kuweza kuwa miongoni mwa wanaostahili kupatiwa fursa za ajira katika migodi sambamba na fursa za utoaji huduma katika miradi hiyo.
Pamoja watoa huduma wote kuhakikisha wanatoa huduma bora kulingana na viwango stahiki ili kuendelea kuaminika katika utoaji wa huduma husika.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...