-Tume Ya Madini Yaeleza Mzabuni Kuendesha Minada ya Kimataifa Amepatikana
-Wazalishaji wa Chumvi Lindi kicheko, Februari Kiwanda kuanza Kazi
Na Wizara ya Madini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba ameongoza kikao cha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake kupitia na kujadili hatua za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa Bungeni na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akiwasilisha Hotuba yake kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.
Katika Mwaka wa Fedha 2025/26, Wizara ya Madini pamoja na kuweka mikakati ya kutekelezwa, ilipanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali; kuongeza mchango wa Sekta kwenye Pato la Taifa; kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini; kuimarisha uendelezaji minada na maonesho ya madini ya vito, kuongeza uwekezaji kwenye tafiti zake za kina; kuwarasimisha wachimbaji wadogo na kuzijengea uwezo taasisi zake.
Akizungumza katika kikao hicho, Eng. Samamba amesisitiza kutekelezwa kikamilifu kwa ahadi zilizotolewa na Wizara ili kuendelea kuongeza tija kwa taifa kupitia rasilimali madini.
Naye, Katibu Mtendaji Tume ya Madini Eng. Ramadhan Lwamo amesema tayari mzabuni atakayesimamia minada ya kimataifa ya Madini ya vito amekwishapatikana. Kufanyika
kwa minada ya kimataifa ya Madini ya vito pamoja na mambo mengine kutaongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kupitia fedha za kigeni, kuitangaza Tanzania na madini yake yanayopatikana nchini, kuvutia uwekezaji zaidi, kuimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa kupitia minada hiyo ya madini ya vito, kuwepo kwa bei halisi ya soko, uwazi na kuongeza washiriki wa ndani na kimataifa.
Manufaa mengine ni pamoja na kukuza wachimbaji wa ndani, masoko ya uhakika ya madini ya vito na bei za uhakika.
Pamoja na masuala mbalimbali yaliyojadiliwa, taarifa ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imeeleza kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kiwanda cha kusafisha chumvi katika Mkoa wa Lindi ambapo imeeleza kwamba matarajio ni kuwa ifikapo mwezi Februari, 2026 kiwanda hicho kitaanza kazi na hivyo kuondoa changamoto ya soko kwa wazalishaji wa chumvi.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...