Dar es Salaam, Tanzania | Jumanne, 24 Februari 2026 - Benki ya Stanbic Tanzania imetambulisha rasmi huduma ya Lipa Simpo kwa wateja, ikiruhusu kufanya malipo moja kwa moja kupitia Stanbic App au USSD *150*29#.

Hii inakuja baada ya mfumo wa Lipa Simpo kuwepo kwa muda, ukiruhusu wajasiriamali na biashara kupokea malipo kupitia QR kutoka benki na mitandao yote nchini.

Kupitia huduma hii ya ufanyaji malipo, wateja wanaweza kulipa bidhaa na huduma kwa sekunde chache, salama na moja kwa moja kutokea kwenye akaunti zao za Benki ya Stanbic, bila kuhitaji pesa taslimu au kubeba chenji.

Akizungumza akiwa Mwenge Dar es Salaam leo, katika ziara maalum ya kutembelea wateja na kutoa elimu juu ya huduma hii, Mkuu wa Huduma za Kidijitali, Stanbic Bank, Edward Balandya amesema kuwa: “Kwa kipindi maalum hadi Aprili 2026, miamala ya zaidi ya TZS 40,000 itatozwa ada ya TZS 1,000 tu, ikiruhusu wateja kulipa kiasi kikubwa kwa gharama ndogo.”

“Tunawashauri wateja kupakua Stanbic App ili kuanza kutumia Lipa Simpo na kufurahia malipo haraka, salama na rahisi.”

Aliendelea kusema “Tumeanzisha kampeni za uhamasishaji katika maeneo yenye shughuli nyingi za kibiashara jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, zinaonyesha matumizi ya moja kwa moja ya Lipa Simpo ambayo inatoa suluhisho la malipo kwa kutumia QR Code. Kampeni hizi pia zinalenga kukusanya mrejesho kutoka kwa wateja na wafanyabiashara wanaotumia huduma hiyo”.

Kwa upande wake, Dickson Senzi, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano wa Benki ya Stanbic Tanzania, alieleza kuwa kupunguza utegemezi wa fedha taslimu kunasaidia kuongeza uwazi, kupunguza hatari za upotevu na kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), ambazo ndizo mhimili wa uchumi wa Tanzania.

“Kampeni zetu si za maonyesho tu. Bali ni utekelezaji wa vitendo unaoonesha jinsi malipo ya kidijitali yanavyofanya kazi katika shughuli za kila siku za kiuchumi, kuanzia manunuzi ya rejareja hadi miamala ya kibiashara. Leo hii, malipo yako mikononi mwako kupitia majukwaa salama ya kidijitali yanakuongezea uhakika wa pesa yako kuwa salama. Kama benki, tunapaswa kuendana na hali hiyo na kuhakikisha suluhisho zetu zinapatikana, zinakidhi gharama na zinaaminika,” aliongeza Senzi.

Kwa kuunganisha upanuzi wa huduma za mawakala wa benki, malipo kwa kutumia QR Code na punguzo la gharama nafuu, Benki ya Stanbic Tanzania inaendelea kujipambanua kama kinara katika mabadiliko ya kidijitali nchini.

Meneja Mwandamizi wa  Mawasiliano wa Benki ya Stanbic,  Dickson Senzi (kushoto), na Meneja wa Kidijitali na Biashara Mtandaoni wa benki hiyo, Godlisten Shirima (kulia), wakimuonyesha Malipula Suti (katikati)  jinsi ya kupokea malipo kupitia LIPA SIMPO na kusisitiza kasi, usalama na gharama nafuu ya suluhisho za malipo ya kidijitali za Stanbic kwa biashara za ndani. Ziara ya kutembelea maduka yanayotumia huduma hiyo lilifanyika  jijini Dar es salaam jana.
Mkuu wa Idara ya Kidijitali na Biashara Mtandaoni Benki ya  Stanbic  Tanzania, Edward Balandya (watatu kushoto) pamoja na  Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano, Dickson Senzi (wapili kushoto)  wakiongea  mfanyabiashara eneo la Mwenge wakati wa ziara ya kutembelea wafanyabishara na kuangalia jinsi ya kupokea malipo kupitia LIPA SIMPO ya benki hiyo na kusisitiza kasi, usalama na gharama nafuu ya suluhisho za malipo ya kidijitali za Stanbic kwa biashara za ndani.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...