Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM na Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemuagiza Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kufanya utafiti wa kina na kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chakula unaoikabili Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

Maagizo hayo ameyatoa leo Februari 5, 2026, wilayani Chemba, akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hatua hiyo imekuja kufuatia ombi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Chemba pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, wakieleza hali ngumu ya upatikanaji wa chakula na bei kubwa zisizolingana na kipato cha wananchi.

Dkt. Nchimbi amesema kwa kuwa suala hilo liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, akisisitiza kuwa utafiti wa haraka unahitajika ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo na kujiridhisha iwapo changamoto ya uhaba wa chakula inaingia katika eneo la maafa linalohitaji hatua za dharura za Serikali.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Chemba, Kunti Majala, wakati akitoa salamu za Jimbo hilo kwa mgeni rasmi, amesema wananchi wa Chemba wamekuwa wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kufuatia hali mbaya ya kilimo iliyojitokeza mwaka uliopita, hali iliyosababisha mavuno kuwa machache.

Majala amesema kwa sasa gunia moja la mahindi linauzwa kati ya shilingi laki moja na elfu ishirini, bei ambayo wananchi wengi hawawezi kumudu kutokana na uchumi wa wilaya hiyo kutegemea zaidi kilimo, huku wakulima wengi wakishindwa kupata mazao ya kutosha ya kuuza ili kupata kipato cha kuendesha familia zao.

Kutokana na hali hiyo, Mbunge huyo alimuomba Dkt. Nchimbi, ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, kuwasaidia  kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), ili wananchi waweze kununua chakula kwa bei nafuu.

Maagizo hayo ya Makamu wa Rais yamepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Chemba, ambao wanaamini kuwa hatua za haraka kutoka Serikalini zitasaidia kupunguza makali ya uhaba wa chakula na kurejesha ustawi wa maisha yao, huku wakisubiri matokeo ya utafiti na maamuzi yatakayofikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...