📍Yataja utendaji wake kama kiungo muhimu kwenye chama na serikali

*NA MWANDISHI WETU, MBEYA

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Vijijini, imemtunukia Tuzo maalum ya Heshima na Shukrani Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Solomon Itunda, kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kuunganisha Serikali na Chama katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Tuzo hiyo imekabidhiwa jana tarehe 26 Februari 2026, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya kilichopokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2025.

Akisoma maelekezo ya Kamati ya Siasa mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Hakimu Mwalupimbi, amemuelezea DC Itunda kama "Kiungo" madhubuti ambaye amekuwa akipatikana wakati wote kushughulikia kero za wananchi na mahitaji ya Chama bila kujali muda.

"DC Itunda umekuwa kiungo kikubwa baina ya Chama na Serikali. Iwe usiku wa manene, asubuhi au mchana, umekuwa ukipokea simu na pale unapokuwa na majukumu mengine unajibu kwa ujumbe mfupi na baadaye unapiga simu kufuatilia. Hiyo ni ishara ya kiongozi aliyelelewa na kukomaa ndani ya Chama," alisema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti aliongeza kuwa uzoefu wa DC Itunda uliotukuka—kuanzia nafasi ya Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya hadi ngazi ya Taifa—umechangia kwa kiasi kikubwa utulivu na mafanikio yanayoonekana sasa wilayani humo.

 Alisisitiza kuwa tuzo hiyo ni ishara ya upendo na shukrani kutoka kwa wana-CCM ili kumtia moyo aendelee kukibeba Chama, hususan katika nyakati hizi za kuelekea majukumu mazito ya kitaifa.

Akizungumza kwa unyenyekevu baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa malezi yaliyomfikisha katika nafasi hiyo ya utumishi wa umma.

Kamati ya Siasa ya Wilaya imebainisha kuwa utaratibu huo wa kutambua na kupongeza watendaji wanaofanya vizuri utakuwa endelevu ili kuongeza ari ya utumishi ndani ya Wilaya ya Mbeya.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...