Na OWM - TAMISEMI, Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mhe Cecilia Daniel Paresso amesisitiza ushirikishwaji wa wananchi wakati wa utungaji na uhuishaji wa Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuwajengea wananchi uelewa wa sheria hizo ambao utawezesha utekelezaji wake katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mhe. Paresso ametoa wito huo wa ushirikishwaji wa wananchi katika utungaji wa sheria ndogo leo Februari 10, 2026 Jijini Dodoma, wakati akiongoza Kikao cha Mafunzo kwa kamati yake kuhusu Sheria Tatu za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na uhusiano wake na sheria ndogo za Mamlaka hizo.

Mhe. Paresso na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wameishauri Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kufanya mapitio ya Sheria Ndogo ambazo zimepitwa na wakati ili kuzihuisha au kuziondoa sheria zitakazobainika kutotekelezeka.

Akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesema Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI itawashirikisha wananchi wakati wa kutunga Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa kama kamati ilivyoelekeza, lengo likiwa ni kuwajengea uelewa wananchi na kuwezesha utekelezaji wake.

Aidha, Mhe. Mmuya ameiahidi kamati hiyo kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI itafanya mapitio ya Sheria Ndogo za Mamlaka za Mitaa ili kujiridhisha kama zinakwenda na wakati, na kuongeza kuwa itazihuisha na kuziondoa sheria ambazo zitakazobainika kupitwa na wakati.

Katika kikao kazi hicho cha mafunzo, wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wamepata fursa ya kupitia Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...