Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
KATIKA kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu vya tiba na ugumu wa lugha kwa wanafunzi, Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) kwa kushirikiana na Mhadhiri wa chuo hicho, Profesa David Ngasapa, wamechapisha vitabu vya anatomia ili kuongeza uelewa wa wanafunzi na kufanya rejea wawapo katika kliniki.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 25, 2026 jijini Dar es Salaam, Profesa Ngasapa ambaye ni mwandishi wa vitabu hivyo, alisema anatomia ni somo la msingi kwa daktari kwani ndipo anaufahamu mwili wa binadamu unavyofanya kazi.

Alisema ameamua kuandika vitabu vinavyozingatia mfumo wa elimu unaolenga umahiri (Competence-Based Education), ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa udaktari hapa nchini.

“Moja ya sababu kuu iliyonisukuma kuandika vitabu hivi ni upatikanaji mdogo wa vitabu vya rejea, hali inayowalazimu wanafunzi kutegemea ‘notisi’ za walimu ambazo hutofautiana kutoka mwalimu mmoja hadi mwingine,” alisema Profesa Ngasapa.

Alieleza kuwa vitabu vingi vya zamani viliandikwa kwa lugha ngumu ya Kiingereza na waandishi ambao Kiingereza ni lugha yao ya kwanza, tofauti na wanafunzi wa Tanzania ambao kwao ni lugha ya tatu.

Amesema moja ya vitabu kinaangalia mimba inavyotungwa hadi mtoto anavyozaliwa na mabadiliko ya mwili wa binadamu yanavyotokea, vyanzo na sababu zake.

Alisema zamani kulikuwa na upungufu wa vitabu vya somo hilo nchini lakini kwa sasa havipatikani kabisa, na kwamba chuoni hapo kulikuwa na kitabu kimoja cha anatomia ambacho wanafunzi walitumia kutoa nakala.

“Mbali na uhaba wa vitabu hivi, sababu nyingine iliyonisukuma kuandika vitabu hivi ni kutumia lugha rahisi na yenye kueleweka ya Kiingereza, kuendana na mtaala wa sasa wa umahiri na kuhimiza wanafunzi kuelewa badala ya kukariri,” alieleza.

Alifafanua kuwa wanafunzi wanahangaika kuelewa lugha kabla hata ya kufahamu dhana, huku mifano inayotolewa katika baadhi ya vitabu vya zamani ikiendelea kuwatatanisha.

“Wanafunzi wanahangaika kuelewa lugha yenyewe kabla hata ya kufahamu dhana. Pia mifano inayotolewa inazidi kuwatatanisha. Mfano, wanaeleza mfuko wa nyongo una umbo la ‘pear’, lakini pears za Ulaya ni tofauti na za Njombe au Iringa. Hivyo mwanafunzi anashindwa kupata picha halisi,” alisema.

Alisema vitabu vipya vimeandikwa kwa lugha rahisi na mifano inayoendana na mazingira ya wanafunzi wa Afrika Mashariki ili kusaidia uelewa badala ya kukariri.

Alibainisha kuwa vitabu hivyo vimeandaliwa kwa kuzingatia mfumo wa elimu unaolenga umahiri, tofauti na mfumo wa zamani uliokuwa unahamasisha kukariri.

“Mitaala yetu sasa inazingatia umahiri. Lakini unakuta mitaala inasema hivi, vitabu vinasema kitu kingine. Sisi tumeandaa vitabu vinavyoendana moja kwa moja na mfumo wa sasa, ili mwanafunzi aelewe na aweze kutumia maarifa yake kliniki,” alisema.

Alisisitiza kuwa lengo ni kuzalisha madaktari bora zaidi, kwa kuwa anatomia ni somo la msingi linalomjengea mwanafunzi uelewa wa mwili wa binadamu kabla ya kuingia kwenye mafunzo ya kliniki.

Akizungumzia muda wa kuandaa vitabu hivyo, Profesa Ngasapa alisema mchakato wa kuandika moja kwa moja ulichukua takribani miaka mitatu, huku maandalizi, utafiti na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ya kufundisha vikichangia kukamilika kwa kazi hiyo.

Alikiri kuwa changamoto kubwa ilikuwa kuandika wakati akiendelea na majukumu ya kufundisha na kufanya utafiti, pamoja na kuandaa michoro ya kitaalamu inayohitajika katika somo la anatomia.

“Ni somo gumu, linahitaji michoro mingi na maandalizi makubwa. Kutayarisha michoro ilikuwa kazi ngumu sana,” alisema.

Alifafanua kuwa gharama za uchapishaji kwa vitabu viwili vya awali zilifikia takribani shilingi milioni 29, zikigharamiwa na MUHAS. Hata hivyo, chuo kitapanga bei itakayoongeza kiasi kidogo juu ya gharama za uzalishaji ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.

“Hatutaki kila wakati kuomba fedha chuoni. Fedha zitokanazo na mauzo zitatumika kuchapisha nakala nyingine kwa wanafunzi wanaokuja,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa kuna mpango wa kuvitoa vitabu hivyo katika mfumo wa kidijitali siku zijazo, sambamba na mwelekeo wa dunia kuelekea kwenye teknolojia.

Alisema tayari chuo kimechapisha zaidi ya nakala 400 na wamepokea maombi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Zimbabwe na taasisi moja kutoka India iliyoonesha nia ya kununua vitabu hivyo.

Alieleza kuwa tatizo la uhaba wa vitabu vya tiba si la Tanzania pekee, bali linazikumba pia nchi jirani za Afrika Mashariki. Hata hivyo, alikiri kuwa vitabu vya kitaaluma havina faida kubwa kifedha kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi, akitoa mfano fani ya udaktari wa meno inayochukua wanafunzi takribani 60 kwa mwaka.

Kuhusu uendelevu wa taaluma hiyo, alisema tayari ameanza kuwaandaa wahadhiri vijana watakaobeba jukumu hilo siku zijazo, akiwemo Mkuu wa Idara, madaktari na wahadhiri wanaoendelea na masomo ya uzamivu (PhD).

“Hawa ndio watakaokuja kuendeleza kazi hii. Tumewapa uzoefu na tunafanya nao kazi kwa karibu,” alisema.
Naye, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Tiba, Profesa Agricola Joachim, alisema wanajivunia kupata vitabu hivyo ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi na kupata elimu wanayoihitaji.

“Tunampongeza kwa kujitoa, jukumu letu ni kufundisha na kufanya tafiti na yeye ametoa muda wake kuandika na chuo kimempa sapoti kuchapisha vitabu kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji,” alisisitiza.

Alihimiza walimu wengine kuandika vitabu vitakavyowasaidia Watanzania.

Profesa Ngasapa alimaliza kwa kuwasihi wanafunzi na jamii kwa ujumla kutumia vitabu hivyo kikamilifu, akisisitiza kuwa vitawasaidia kupata elimu yenye kuzingatia umahiri na kuwafanya wawe wataalamu bora zaidi katika sekta ya afya.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...