
Na Mwandishi Wetu Morogoro
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa, imefanya kikao kazi kinacholenga kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti katika eneo la usimamizi wa maafa leo tarehe 12 februari, 2026 Mkoani Morogoro.

Akifungua Kikao hicho Dkt. James Henry Kilabuko Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa niaba ya Dkt. Jim Yonazi Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo amesema;

Lengo kuu la kikao kazi hiki ni kuandaa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano na Mpango Kazi wa kuimarisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia, Utafiti na Ubunifu katika usimamizi wa maafa kwa pamoja nchini ili kuweza kuwasaidia Wananchi katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa kipindi yanapotokea.

Aidha ameeleza kwamba, Serikali inadhamira ya kuimarisha mfumo wa taifa wa usimamizi wa maafa kwa kuzingatia mzingo mzima wa maafa unaojumuisha kuzuia na kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na maafa yanapotokea pamoja na kurejesha hali baada ya maafa.

Amesema Mwelekeo huu, umeainishwa wazi katika Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, (Toleo la Mwaka 2025) inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na tafiti katika kufanya maamuzi na utendaji wenye ufanisi.

"Katika utekelezaji wa sera na sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu imeona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti nchini, Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha kuwa tafiti, mafunzo na teknolojia zinajibu changamoto zinazokabili taifa letu" amesema Dkt. Kilabuko

Pamoja na hayo, Dkt. Kilabuko amesisitiza uunganishaji wa nguvu, maarifa na rasilimali tulizonazo, utajenga Taifa lenye ustahimilivu dhidi ya maafa na lenye uwezo wa kufikia malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Menejimentu ya Maafa Brg. Jenerali Hosea M. Ndagala alisema, kikao hiki kinatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja kati ya wahadhiri, wataalamu wa kitaaluma na watendaji wa Serikali kuhusu mahitaji halisi ya shughuli za usimamizi wa maafa katika ngazi ya kitaifa, mkoa hadi wilaya kwa lengo la kuongeza ufanisi wa majibu wakati wa maafa na kuboresha mikakati ya kurejesha hali baada ya maafa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...