Na. Chedaiwe Msuya na Jordan Mbwambo WF, Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mikopo yenye riba kubwa ili kulinda wananchi dhidi ya mikopo hatarishi, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mhe. Munde alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mhe. Nyakisa Sanga, aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wananchi, hususan wafanyakazi, hawabebeshwi mzigo wa riba kubwa za mikopo.

Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na BoT imeendelea kusimamia kwa karibu taasisi za fedha ili kuhakikisha zinazingatia sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa mikopo.

Akijibu swali la msingi lililoulizwa kuhusu wakati ambao wafanyakazi wa Tanzania watapunguziwa riba za mikopo na kufikia asilimia 7 au 8, Mhe. Munde alisema kuwa kwa mujibu wa sera za uchumi wa nchi, riba za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha huamuliwa na nguvu za soko, hivyo Serikali haiwezi kuelekeza moja kwa moja taasisi hizo kuweka viwango maalum vya riba kwa kundi fulani la wakopaji.

“Riba za mikopo nchini huamuliwa na soko. Serikali ikielekeza taasisi za fedha kuweka kiwango maalum cha riba kwa wafanyakazi au mkopaji yeyote, itakuwa inakinzana na mwelekeo wa sera ya soko huria,” alisema Mhe. Munde.

Mhe. Munde alifafanua kuwa taasisi za fedha zina uhuru wa kuweka viwango vya riba vya chini ikiwemo asilimia 7 au pungufu endapo zitaona inafaa kufanya hivyo.

Aidha, wafanyakazi binafsi au kupitia waajiri wao wana fursa ya kufanya majadiliano na benki husika ili kukubaliana juu ya viwango vya riba vinavyoweza kutolewa.

Mhe. Munde alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kifedha nchini kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu na yenye tija kwa wananchi, huku ikilinda misingi ya sera ya soko huria inayotumika nchini.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Kiamboni, Mhe. Nyakisa Sanga, pamoja na swali la msingi kuhusu riba za mikopo kwa wafanyakazi, bungeni jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...