Na FARIDA MANGUBE MOROGORO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imewataka walipakodi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro kuanza kuuzoea na kuutumia Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Kodi za Ndani wa Kielektroniki (IDRAS), unaolenga kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa kodi kwa njia ya kisasa, rahisi na yenye ufanisi zaidi.
Akizungumza na walipakodi na wadau wa kodi mkoani humo Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka TRA makao makuu Bi. Ernesta Shirima, amesema mfumo wa IDRAS unakwenda kuchukua nafasi ya mifumo mbalimbali inayotumika kwa sasa ndani ya TRA, hatua itakayowezesha kuimarisha utoaji wa huduma za kodi kwa njia ya kidijitali.
Bi. Ernesta amesema kuwa utekelezaji wa IDRAS utaleta mapinduzi makubwa kwa kuondoa matumizi ya huduma za makaratasi (manual) na kuwezesha shughuli zote zinazohusiana na usimamizi wa kodi za ndani kufanyika kwa njia ya kielektroniki.
“Mfumo huu utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi na kurahisisha huduma kwa walipakodi pamoja na watumiaji wengine wa TRA. Lengo letu ni kuwa na mfumo mmoja uliounganishwa, unaorahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza usumbufu uliokuwepo awali,” amesema.
Ameongeza kuwa IDRAS inalenga kuboresha kwa ujumla huduma za usimamizi wa kodi za ndani, kupunguza matumizi ya mifumo mingi isiyounganishwa na kuongeza uwazi, ufanisi na urahisi kwa walipakodi na wadau wote wa kodi.
Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Kodi wa Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, Bw. John Magembe, amesema kuwa TRA imewawezesha walipakodi na watumiaji wengine kuufikia mfumo wa majaribio (Test System) wa IDRAS ili kujifunza na kuuzoea mfumo huo kabla ya kuanza kutumika rasmi.
“Kipindi hiki cha mpito kinawapa walipakodi fursa ya kufanya majaribio, kujifunza matumizi ya mfumo na kupata uelewa wa kina kabla ya uzinduzi rasmi wa IDRAS,” amesema Bw. Magembe.
Naye Afisa Msimamizi wa Kodi wa Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, Bw. Nickson Mugonya, amesema kuwa mfumo wa IDRAS umejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hatua itakayoboresha utoaji wa huduma na kuleta manufaa makubwa kwa walipakodi na jamii kwa ujumla.
Bw. Mugonya ametaja baadhi ya faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma kwa saa 24 kwa siku, uhifadhi salama wa taarifa na kumbukumbu za kikodi, ufuatiliaji wa maombi kwa njia ya mtandao pamoja na usimamizi wa kodi kwa njia ya kidijitali.
“IDRAS ni chachu ya mageuzi ya kidijitali ndani ya TRA, na tunatarajia itaongeza ufanisi, uwazi na uaminifu katika mfumo mzima wa kodi nchini,” amesema.
TRA imeendelea kuhimiza walipakodi wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo na matumizi ya mfumo huo mpya ili kuhakikisha mpito wa kwenda kwenye mfumo wa kidijitali unakuwa rahisi na wenye mafanikio.



.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...