Na Diana Byera-Bukoba.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Jacob Nkwera, amewahakikishia madiwani wa Manispaa ya Bukoba kuwa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni unatarajiwa kuanza February 28 mwaka huu, baada ya taratibu zote za ukandarasi kukamilika.

Akijibu swali la Diwani wa Kata ya Bilele, Taufiq Saharifu, katika kikao cha Baraza la Madiwani, Nkwera alisema kuwa mradi huo utaanza licha ya mkandarasi kutambulishwa na kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo miezi sita iliyopita. Diwani huyo alitaka kujua ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa.

Nkwera alisema kuwa hatua ya kwanza ilikuwa ni kumpata mkandarasi pamoja na mkandarasi mshauri, hatua ambazo sasa zimekamilika.

Alisema, “Hatua ya kwanza ilikuwa ni kumpata mkandarasi na mkandarasi mshauri, jambo ambalo sasa limekamilika. Matumaini makubwa ni kuwa mradi utaanza kutekelezwa February 28.”

Katika swali lake la msingi, Diwani Saharifu alisema wananchi wa Kata ya Bilele wamekuwa wakihoji ni lini mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni utaanza kutekelezwa, kwani una matumaini makubwa ya kuwaondoa maelfu ya wananchi kwenye adha ya mafuriko.

 Alisema wananchi wamesubiri kwa muda mrefu tangu walipoelezwa kuwa mkandarasi angeanza kazi miezi sita iliyopita.

“Tumepita kuomba kura, wananchi wametuamini, lakini mpaka sasa tunaelekea kuchanganyikiwa kwa sababu hatuoni mkandarasi. Mvua hizi za siku tatu zimeanza kuleta hofu, mafuriko yameanza, wananchi wanapita wakati mgumu, na sisi madiwani tunabanwa sana. Tunashindwa hata kupumua. Tunaomba tusaidiwe mradi uanze.”

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bukoba Mjini, Shabani Mdoe, alisema kuwa chama hicho hakiridhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni, akieleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini ambao wamekuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara.

Mdoe alisema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, iliyonadiwa katika uchaguzi wa mwaka 2025, ilieleza namna serikali ya CCM ilivyopanga kuutekeleza kwa kasi mradi huo.

Alisema, “Kama Chama Cha Mapinduzi tunaomba sana mradi wa kingo za Mto Kanoni utekelezwe. Ni mradi unaogusa watu na maisha yao. Miezi sita ya mkandarasi kukaa kimya ni mingi sana. Tunaomba utekelezaji uanze haraka ili tujue cha kuwajibu wananchi.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, alisema kuwa serikali itaendelea kufuatilia na kuhakikisha mradi huo unaanza mara moja.

Alisema, “Serikali itaendelea kufuatilia na kuhakikisha mradi unaanza mara moja ili kukimbizana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kuanzia February hadi July, ambazo husababisha maafa.”

Mradi wa kusafisha na kujenga kingo za Mto Kanoni ni miongoni mwa miradi ya TACTICS inayopangwa kutekelezwa katika Manispaa ya Bukoba. Mkandarasi wa mradi huo pia anatarajiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 10 pamoja na ufungaji wa taa za barabarani.









 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...