NA MASHAKA MHANDO, Handeni
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Katibu Mkuu Wizara ya elimu, sayansi na teklonojia, kuwachukulia hatua watumishi wa Wizara hiyo waliosimamia ujenzi wa Chuo Cha Veta wilayani hapa na kusababisha mifuko 1,262 ya saruji kuganda.
Sambamba na agizo hilo Waziri Mkuu pia amemwagiza Kamanda wa Takukuru mkoani Tanga, kwenda kufanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha katika jengo la kituo cha afya Sindeni ambako milango 34 ipo chini baada ya mkandarasi kuweka milango hiyo kwa kiwango cha chini.
Akizungumza jana jioni katika ziara yake ya siku ya kwanza mkoani hapa, Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa mkoa kufuatilia la matumizi mabaya ya fedha kwenye miradi hiyo ambayo.
Alisema wilayani Handeni kuna miradi imekuwa na kasoro ambapo jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Sindeni milango ipo chini ya kiwango kutokana na watu kufanya kazi kwa mazoea.
"Kamanda wa Takukuru wote waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria, RC (Mkuu wa mkoa Balozi Dkt Batilda Burihan) Fuatilia wahusika wote kama wameweka milango hiyo kusudi ili wachukue fedha za serikali, wachukuliwe hatua mradi ule ni wa zaidi ya milioni 300," alisema Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu ametaka watumishi ambao wamesimamia ujenzi wa maabara ya Chuo Cha Veta wilayani hapa ambao wamesababisha mifuko hiyo ya saruji kuganda wahakikishe wanarudisha fedha hizo na kama walifanya uzembe wachukuliwa hatua.
"Waliotumwa kujenga Veta ili vijana wasome wamekaa ofisini wakagandisha mifuko 1,262, huu ni uzembe tunasema hatuwezi kuvumilia, nimekuja hapa nikijua ni halmashauri mmefanya hivyo lakini nimeambiwa je go Hilo linasimakiwa na watumishi wa Wizara ya elimu, namwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya elimu awavhukulie hatua na wakatwe fedha kwenye mishahara yao kurejesha ili jengo hilo lijengwe," alisema.
Waziri Mkuu alisema kuwa Sasa watumishi wa serikali waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kuwahudumia watanzania ambao wamekuwa na matumaini makubwa na serikali yao.
Awali wakati akikagua eneo la ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme eneo la Mkata, ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha inatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.9 zilizobaki kwa ajili ya mkandarasi anayejenga kituo cha kupozea umeme (Substation) mjini Mkata, ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo na kupata taarifa kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Mhandisi Lazaro Twange, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya miradi ya umeme ili kuongeza upatikanaji wa Nishati hiyo ipatikane kwa wananchi na wawekezaji.
Ameagiza Wizara ya Nishati, chini ya Waziri Deogratius Ndejembi, kufuatilia kwa ukaribu utoaji wa fedha hizo ili mkandarasi aongeze kasi ya ujenzi, kwani mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa Trilioni Moja zilizotolewa nchi nzima unaolenga kuboresha nishati kwa ajili ya viwanda.
Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameonyesha uungwana na vitendo kwa kutekeleza ahadi zake mapema, katika siku zake 100 za uongozi wake ikiwemo ajira za watumishi 5,000 wa afya na 7,000 wa elimu ndani ya kipindi kifupi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ametoa onyo kali kwa wakandarasi wanaochepusha fedha za miradi kwenda kulipa madeni yao binafsi au kwenye miradi mingine, akisisitiza kuwa Serikali haina mzaha katika suala hilo.
"Tunataka kiasi cha fedha kilichopokelewa kilingane na thamani ya kazi iliyofanyika. Kuna wakandarasi wanatoa namba za akaunti zao za nje ambazo zina madeni, wakilipwa fedha zinakatwa na benki na mradi unakwama. Watu wa aina hiyo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja," alisisitiza Waziri Mkuu.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa jumla ya Shilingi Trilioni 1.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya umeme ipatayo 27 nchi nzima, ukiwemo mradi huu wa Mkata unaolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati kwenye Gridi ya Taifa.
Waziri Ndejembi alisisitiza kuwa ujenzi wa kituo hicho cha kupozea umeme (Substation) ni suluhisho la kudumu kwa wawekezaji, hususan wa viwanda vya madini ya Graphite, ambao hapo awali walikuwa wakisita kuwekeza kutokana na changamoto ya nishati.
"Rais ametoa Trilioni 1.9 kwa ajili ya miradi hii 27 ya umeme nchini. Hapa Mkata tunapeleka umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, na tayari Bilioni 3 zimetolewa kwa ajili ya kubadilisha nguzo za umeme kuelekea Kwamsisi ili kuimarisha miundombinu hiyo,"* alisema Waziri Ndejembi.
Aidha, Waziri huyo wa Nishati ameahidi kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote ili kuhakikisha kazi hizo zinakamilika kwa wakati uliopangwa, akisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa mpya za kiviwanda na kiuchumi kwa mkoa wa Tanga na maeneo jirani.
Mtendaji Mkuu wa TANESCO amebainisha kuwa Serikali inaendelea na uimarishaji wa Gridi ya Taifa mkoani Tanga kupitia miradi miwili mikubwa. Mradi wa Mkata unahusisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme (2X60MVA) na njia ya kilomita 45 kuelekea Kwamsisi.
Mradi huu unagharimu Shilingi Bilioni 49.89 na unatekelezwa na kampuni ya TBEA kutoka China na Central Electricals ya Tanzania kwa lengo la kuimarisha nishati kwenye migodi ya Graphite na viwanda.
Hadi kufikia Februari 2026, ujenzi wa kituo cha Mkata umefikia asilimia 20.37, huku kazi za misingi zikiwa zimekamilika kwa asilimia 55. Kwa upande wa njia ya usambazaji, tayari nguzo zimeshasimikwa kwa urefu wa kilomita 30 kati ya 45 zinazohitajiwa.
Sambamba na hayo, Serikali inatekeleza mradi mwingine wa kimkakati wa "Gridi Imara" kutoka Mkata hadi Kilindi (kV 132) wenye urefu wa kilomita 143.6. Mradi huu unatekelezwa na kampuni ya Kalpataru kutoka India kwa gharama ya Shilingi Bilioni 98.46.
Mpaka sasa, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Kilindi umefikia asilimia 30.9 na kituo cha kupoza umeme asilimia 35.9, huku ununuzi wa mitambo ukiwa umekamilika kwa asilimia 80.
Akijibu kero ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania kuacha kubaguana na badala yake wafuate sheria za nchi zinazoruhusu Mtanzania kuishi popote bila kuvunja taratibu.
Waziri Mkuu amebainisha mambo makuu mawili ambayo ni Mtanzania anaruhusiwa kuishi popote, lakini lazima azingatie Sheria akitambuabkuwa ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu inaongezeka.
Lakini pia alisema kosa la mfugaji mmoja au mkulima mmoja lisiwakilishe jamii nzima bali wananchi waishi kwa kuheshimiana ili kuepusha migongano isiyokuwa na lazima.
Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji isifike wakati ikakosa Utu miongoni mwa jamii hizo hivyo akataka waheshimiane na utatuzi wa migogoro ambayo inatakiwa iamuliwe kwa mujibu wa Sheria.
"Tuambizane na tuchukue hatua haya mambo tukiyaacha yataleta ufa miongoni mwetu, tuchukue mkondo wake kwa mtu binafsi anayevunja sheria na siyo kuanzisha ufa wa utengano," alisema.
Amewaagiza viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Tanga kutofumbia macho rushwa inayochelewesha haki na badala yake wasimamie matumizi bora ya ardhi ili kumaliza mizozo hiyo kwa uungwana.
Waziri Mkuu amesikiliza kero za wananchi nyingine alizitatua papo hapo na nyingine ameagiza mawaziri wa Wizara za kisekta wakae pamoja kupata masuluhisho ya majawabu ya wananchi.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu alikuwa na waziri wa Kilimo Daniel Chongolo ambaye alisema wilayani Handeni ili migogoro ya wakulima na wafugaji iweze kuondoka wameandaa mpango wa matumizi Bora ya ardhi kwa kushirikiana na wizara za Mifugo na ardhi ili kutenga na kuhakikisha makundi hayo yanaishi kwa Amani.
Pia alisema wananchi wa Handeni katika Msimu wa chakula waliweza kulima ufuta, mbaazi na dengu na kupata jumla ya shilingi bilioni 2.7 na kwamba Sasa mpango uliyopo ni kujenga mabwawa ya umwagiliaji katika vijiji sita wilayani humo.
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt Bashiru Ally Kakurwa alisema kuwa yote yaliyoainishwa katika ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030 yatatekelezwa ikiwemo kuweka mpango wa uzalishaji wa mbegu bora za Mifugo na ambari.
Pia alisema kuboresha afya ya Mifugo kwa kutoa chanjo ambayo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuzindua chanjo hizo mwaka jana lakini pia kuboresha sekta ya Uvuvi kwa serikali kununua boti tano na moja itawasili February 21.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za mitaa Tamisemi Profesa Rizik Shemdoe alisema wanamshukuru Rais kwa kuwapatia miradi ya kimkakati katika mkoa wTanga ikiwemo ujenzi wa Majengo ya dharura katika hospitali za wilaya ya Handeni, Pangani na Korogwe.
Mbunge wa Handeni mjini Reoben Kwagwila na Naibu Waziri wa Tamisemi alisema kutoka na furaha ya kupata maji kutokana na mradi mkubwa wa miji 28 ambao itafika wilayani hapa, siku ya uzinduzi ataoga hadharani kutokana na furaha ya kupata maji na kukosa muda mrefu.
Waziri wa maji Jumaa Aweso alisema kuwa jumla ya shilingi bilioni 171 zinagharamia mradi wa Maji wa miji 28 ambao ni katika wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani hivi Sasa umefikia asilimia 75 na kwamba hadi kufikia Machi mwaka huu maji yataanza kupatikana matika maeneo hayo.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...