KAMPUNI ya Utalii ya Zara Tours yenye Makao yake makuu mjini Moshi imeendelea kuthibitisha ubora wake katika sekta ya utalii baada ya kunyakua tuzo nyingine muhimu,ikiwa ni muendelezo wa mfululizo wa tuzo mbalimbali ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizipata karibuni kila mwaka.

Tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa katika hafla kubwa ya Serengeti Awards, iliyofanyika usiku wa kuamkia Leo katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha ,hafla iliyowakutanisha wadau wakuu wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba ambaye aliipongeza sekta ya Utalii kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na Kuongeza ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Akizungumza mara baada ya Kupokea tuzo hiyo,Mkurugenzi wa Zara Tours, Zainab Ansell alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa ,mshikamano wa timu na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa sekta ya utalii hususani katika kulinda na kuendeleza vivutio vya Taifa kama Mlima Kilimanjaro.

"Mafanikio yanayoonekana katika Mlima Kilimanjaro ni ushahidi wa wazi wa kazi kubwa iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii hata hivyo Mazingira ya Mlima yameimarika,huduma zimeboreshwa na hali ya usalama imeongezeka kwa kiwango kikubwa jambo linalowapa watalii uzoefu wa kipekee"

Aliongeza kuwa kupitia maboresho hayo Mlima Kilimanjaro umeendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuifanya nchi kuwa moja ya vituo vinavyoongoza kwa utalii wa mlima barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,ongezeko la watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro limechangia kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii na kuongeza mapato ya Taifa huku Kampuni kama Zara Tours zikichukua nafasi muhimu katika kuhakikisha wageni wanapata huduma zenye viwango vya kimataifa.

"Ninajivunia sana mafanikio haya,na Leo siku ya kusherehekea hatua tulizofikia ,Mimi pamoja na timu yangu tumejipanga kikamilifu kuendelea kuboresha viwango vya kitaaluma,kuongezeka ubunifu na kuhakikisha wageni wengi zaidi wanavutiwa kuja kuupanda Mlima Kilimanjaro"

Zainabu aliahidi kuwa Zara Tours itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Serikali katika kukuza utalii endelevu,kulinda mazingira,na kulitangaza Taifa la Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Hafla ya Serengeti Awards imelenga kutambua kuthamini mchango wa taasisi,makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...