TAASISI isiyo ya kiserikali ya Afya ya Mama Foundation imekabidhi mikoba ya vifaa vya kujifungulia wajawazito katika vituo vya afya vya Kimbiji na Mwasonga, wilayani Kigamboni, mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha uzazi salama.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo leo Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo, Felister Bwana, alisema hatua hiyo inathibitisha dhamira ya pamoja ya kulinda maisha ya mama na mtoto mchanga kuhakikisha kila mwanamke anapitia ujauzito na kujifungua kwa heshima, salama na matumaini.
"Nchini Tanzania tumeshuhudia maendeleo ya kutia moyo katika afya ya uzazi kutokana na juhudi za serikali , wahudumu wa afya, washirika wa maendeleo na jamii kwa ujumla.Mafanikio haya yanatuonesha kushirikiana inawezekana,"amesema Felister.
Ameeleza,Afya ya Mama Foundation inatambua wanawake na watoto wachanga wengi wako katika hatari kwa sababu zinazozuilika hususan changamoto wakati wa ujauzito, kujifungua, kuchelewa kupata huduma, upungufu wa vifaa muhimu hasa katika maeneo yenye rasimilali chache.
"Ndiyo maana tumeamua kukabidhi vifaa hivi vya kujifungulia ambavyo vinaweza kuonekana rahisi lakini vinathamani kubwa kwani vinawakilisha maandalizi, usalama na huduma bora katika kujifungua, kupunguza hatari za maambukizi na kuwasaidia wahudumu wa afya kutoa huduma bora zaidi,"amesema Felister.
Amesema, vifaa hivyo pia vinatuma ujumbe muhimu kwa kila mama kuwa hayuko peke yake kwani afya yake na maisha yake ni muhimu.
"Napenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa uongozi wake endelevu na dhamira ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Juhudi hizi ndiyo msingi unaowezesha taasisi kama hii kushirikiana na kuchangia maendeleo haya,"amebainisha.
Awali Mwanzilishi wa Afya ya Mama Foundation, Nkela Makoko, alisema taasisi hiyo inatambua umuhimu wa vifaa hivyo kwa wajawazito kwani baadhi wanashindwa kuvipata wakati wa kujifungua.
"Lengo letu kuu ni kusaidia huduma za mama na mtoto katika kipindi chote cha ujauzito, kujifungua na maendeleo yake baada ya kujifungua. Vifaa hivi vimetolewa na wadau wetu walio guswa na afya ya mama na mtoto,"ameeleza Nkela.
Ameishukuru serikali chini ya Rais Dk. Samia, kuboresha huduma za mama na mtoto hali inayopunguza athari za uzazi kabla, wakati na baada ya kujifungua.
Mganga wa Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mwasonga, Miriam Issa, ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa vifaa hivyo kwa wajawazito ambavyo amesema ni mahitaji muhimu wakati wa kujifungua.
Wanufaika wa vifaa hivyo ambao ni wajawazito, wamesemavifaa hivyo ni zawadi muhimu kwao kwani baadhi yao wanapata changamoto ya kumudu mahitaji yote wakati wa kujifungua.
"Wajawazito tunapata shida unapofika wakati wa kujifungua. Tunashukuru Afya ya Mama Foundation kwa kutukumbuka kutupa vifaa hivi,"alisema Tachael Paul.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...