NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Help to Help East Africa imeendesha mafunzo ya siku 14 kwa wasichana 150 kutoka mikoa 20 nchini, ikiwa na lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Mafunzo hayo yanawalenga zaidi wasichana waliopo vyuoni pamoja na waliohitimu masomo yao, ili kuwajengea uwezo wa kitaalamu unaohitajika katika ajira za kisasa.
Tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2015, tayari umewafikia takribani vijana 11,000 nchini, wakiwemo wanafunzi wa vyuo na wahitimu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa Mradi wa taasisi hiyo, Epifania Muhagama, amesema mradi huo unalenga kuwasaidia wasichana wasio na ujuzi wa awali wa TEHAMA kwa kuwapatia maarifa muhimu kama uandishi wa ripoti, uchambuzi wa data, matumizi ya barua pepe, akili mnemba (AI), pamoja na matumizi ya kompyuta kwa ujumla.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake katika soko la ajira bado uko chini, hali inayochangiwa na kukosa kujiamini pamoja na ukosefu wa ujuzi unaohitajika.
“Mradi huu umeanzishwa baada ya tafiti kubaini kuwa wanawake wengi hawajiamini na hawana ujuzi wa kuwasaidia kupata ajira,” amesema Muhagama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendelezaji TEHAMA kutoka Tume ya TEHAMA na Tafiti iliyo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Gerson Ndanguzi, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea wanawake fursa za kidijitali na kusaidia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa ujuzi huo unalenga kuwasaidia washiriki kutumia TEHAMA kwa usahihi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Aidha, Ndanguzi amewahimiza wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa watu wengi zaidi, akibainisha kuwa bado kuna idadi kubwa ya wananchi ambao hawajafikiwa.
Pia amewasisitiza washiriki kuendelea kujifunza zaidi hata baada ya mafunzo hayo, badala ya kuridhika na ujuzi walioupata pekee.
Naye mnufaika wa mafunzo hayo, Shalom Kokonyo, amesema anatarajia kujifunza ujuzi wa kompyuta, uongozi pamoja na uwekezaji ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yake.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku 14, yakihitimishwa Aprili 1, 2026, ambapo wataalamu kutoka kada mbalimbali za ajira watashiriki kama wazungumzaji.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...