Na; Mwandishi Wetu, Unguja
TIMUya Kwahani FC imetwaa ubingwa wa Masauni Cup baada ya kuichapa Mwembeladu FC kwa changamoto ya mikwaju ya penati 1-0 baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na kujinyakulia kombe pamoja na kitita cha shilingi milioni tano.

Kwahani FC ndio walitangulia kupata bao katika muda wa kawaida lililofungwa na Abdalla Himidi kabla ya Mwembeladu FC kusawazisha dakika za jioni likifungwa na Tariq Mzee na kuzifanya timu hzio kwenda kwenye mikwaju ya penati.

Penalti ya Mundhir Omar Hassan ndio iliyoipa ubingwa Kwahani FC ambayo ilitinga fainali kwa kuichapa Kwalinatu FC bao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali wakati Mwembeladu FC iliyojinyakulia kombe na shilingi 2,000,000 ilipenya kwa penati 3-1 dhidi ya Kiswandui.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma amesema wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa soka nchini ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia mchezo huo yanafikiwa, sambamba na kuwapatia fursa za ajira ndani na nje ya Zanzibar.

Mhe. Riziki amesema Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ina dhamira ya dhati ya kuona mpira wa miguu unakuwa chombo cha kuwainua vijana kiuchumi pamoja na kuwawezesha kujenga mustakabali wao.

Alisema lengo la Rais ni kuhakikisha vijana wa Zanzibar wanatumia vipaji vyao vya soka kupata ajira na kujitambulisha kimataifa, kama ambavyo baadhi ya wachezaji wameanza kufanya, akitolea mfano wa mchezaji Feisal Salum ambaye amekuwa kielelezo cha mafanikio kwa vijana wanaocheza mpira wa miguu.

“Tunataka kuona vijana wengi zaidi kama kina Feisal Salum wanaibuka na kupeperusha bendera ya Zanzibar ndani na nje ya nchi kupitia mchezo wa mpira wa miguu,” alisema Waziri huyo.

Alieleza kuwa kutokana na dhamira hiyo, Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya michezo katika wilaya na mikoa mbalimbali ili kutoa fursa kwa vijana wengi kushiriki michezo na kuendeleza vipaji vyao.

Aidha, alisema mashindano ya soka yanayoandaliwa katika majimbo yana mchango mkubwa katika kuibua vipaji vipya na kuwapa vijana sehemu sahihi ya kutumia muda wao kwa shughuli zenye manufaa badala ya kujihusisha na mambo yasiyofaa.

“Uwepo wa mashindano haya ni jambo zuri kwa sababu yanawawezesha vijana kukutana, kushindana na pia kuimarisha vipaji vyao, hata wazo la kuwa na timu za taifa za majimbo ni zuri kwani litasaidia kuongeza ushindani na kuimarisha maendeleo ya soka,” alisema.

Aliongeza kuwa mashindano hayo pia yanasaidia kujenga mshikamano na uelewano miongoni mwa vijana kutoka maeneo mbalimbali, jambo ambalo ni muhimu katika kuimarisha umoja na maendeleo ya jamii.

Kutokana na hilo, alimpongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa juhudi zake za kuanzisha mashindano hayo akisema hatua hiyo imewasaidia vijana wengi kujikita katika michezo na kujiepusha na vitendo visivyofaa katika jamii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema mashindano hayo yameanzishwa kwa lengo la kuwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao pamoja na kuwaunganisha vijana wa jimbo hilo kupitia michezo.

Mbali na hilo, alisema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga umoja, mshikamano na nidhamu miongoni mwa vijana, hivyo ni vyema kwa jamii kuendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza sekta ya michezo katika ngazi za chini.

Alieleza kuwa kupitia mashindano hayo vijana wengi wamepata nafasi ya kuonekana na kuonesha uwezo wao, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kufikia malengo yao ya kuwa wachezaji bora na hata kupata fursa ya kucheza katika timu mbalimbali za ndani na nje ya Zanzibar.

Aidha, aliwataka vijana wanaoshiriki mashindano hayo kuzingatia nidhamu, kuheshimu sheria za mchezo na kudumisha mshikamano ili mashindano hayo yaweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...