Machi 5 2025, wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya matendo ya huruma kwa jamii inayowazunguka kwa kutembelea Kituo cha Afya Mlali kilichopo Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Ikiwa ni sehemu ya kusambaza upendo kwa jamii, wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe wamekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali pamoja likiwemo tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 5,000 ili kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama katika kituo hicho.

Mbali na tanki hilo, wanawake hao wametoa vifaa tiba, sabuni za maji, vifaa vya kuwekea uchafu (dustbins), vizolea uchafu, mifagio, pampers za watoto na vitambaa vya kufutia watoto (wipes) pamoja na vinywaji kwa wagonjwa. Wanawake hao wametoa vifaa hivyo kwa lengo la kuboresha mazingira ya utoaji huduma pamoja na kuwafariji wagonjwa katika kituo hicho.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema Chuo kimekuwa kikiadhimisha siku hii kwa kufikia jamii zenye uhitaji.

“Kwa takribani miaka nane sasa, Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa kikiadhimisha siku hii, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kaulimbiu ya Chuo, “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.”

Aliongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050,” inalenga kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, siasa na uchumi.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, aliwataka wanawake kuendelea kushirikiana na kusaidiana katika jamii huku akisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Prof. Elizabeth Lulu Genda, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali na kuimarisha maisha ya wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya kituo hicho, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mlali, Dkt. Celestine Luzinga, aliwashukuru wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa msaada wao, akisema vifaa hivyo pamoja na tanki la maji vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mazingira ya utoaji huduma kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa afya.

Baadhi ya akina mama waliopokea zawadi walisema: “Tunashukuru sana kwa msaada huu, hakika huu ni upendo na mmetutiq moyo sana.”

Ziara hii ni mfano wa jinsi wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe wanavyoshirikiana na jamii kuendeleza mshikamano, kusaidia wenye uhitaji, na kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii.

Vilevile, ziara inaashiriaa jinsi wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe wanavyoshirikiana na jamii kuendeleza mshikamano, upendo, kusaidia wenye uhitaji na kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...