Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Ephraim Balozi Mafuru kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii ameongoza timu ya wizara hiyo kwenye kikao cha mkakati na viongozi wa wizara ya Utalii kutoka Jamhuri ya Zambia huku Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikijinasibu kwa upekee wa vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo ambayo asili, urithi na maajabu yanakutana eneo moja.
Mkurugenzi Mafuru ameeleza ujumbe huo kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Waasisi wa Tanzania na Zambia kuunganisha mshikamano wa kiuchumi na kijamii.
Mafuru amesema Tanzania inasonga mbele katika sekta ya utalii kutokana na kuimarisha uhifadhi,miundombinu ya utalii pamoja na utafutaji wa masoko ya kimkakati ndani na nje ya nchi.
Akitoa wasilisho la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Afisa Masoko Mwandamizi Selestine Saitabau alisema Ngorongoro ni kama kikapu cha zawadi ambapo kimebeba vivutio vingi kuanzia historia ya chimbuko la binadamu, wanyamapori, mazalia ya Nyumbu, mchanga unaohama, misitu, ndege, hali ya hewa ya kuvutia na uoto wa asili wenye mandhari yanayonawirisha ikolojia ya Ngorongoro, Serengeti hadi Masai Mara.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru aliwashukuru wageni hao wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Kiongozi na katibu Mkuu wa wizara ya Utalii Zambia na kuwaeleza kuwa Ngorongoro ina sifa zote za kuwa Bustani ya Eden na kuwahakikishia wageni hao kuwa wamerudi nyumbani kwenye asili ya Mababu zao wa takriban miaka zaidi ya milioni 3 iliyopita.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...