Na. Jacob Kasiri - Serengeti

Kauli ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa ni darasa katika shughuli za ulinzi wa maliasili na eneo maarufu duniani kwa ajili ya utalii endelevu imeendelea kukita mizizi katika hifadhi hiyo iliyobeba umaarufu duniani kwa uhamaji wa nyumbu imedhihirika leo machi 17, 2026 baada ya kupokea Ujumbe Maalumu wa Wizara ya Utalii, Idara ya Hifadhi za Taifa na Wanyamapori (DPNW) ya Serikali ya Zambia.

Ujumbe huo ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Mhe. Siazongo Siakalenge ambaye pia anashughulikia masuala ya Fedha na Maendeleo ya Uchumi - Zambia alisema Hifadhi ya Taifa Serengeti ndio eneo sahihi kwao kujifunza namna uhifadhi na utalii ulivyoimarishwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Siakalenge aliongeza; “Licha ya mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri kwa kiasi kikubwa Hifadhi za Taifa Duniani na Zambia ikiwa ni miongoni mwao lakini Hifadhi     ya Taifa Serengeti imeendelea kushamiri, tumeona wanyama wa kila aina, mimea na majani yamestawi huku maji yakiwa ya kutosha. Haya na mengine mengi tuliojifunza kwenu yametufungua macho na tunaenda kuyafanyia kazi.”

“Shughuli za utalii zinazofanyika Serengeti nyingi zinafanana na za Zambia isipokuwa utalii wa Puto (baloon) huu hatuna na katika ziara hii nimeuona na kuuonja, hivyo nasi tunaenda kuuanzisha pia”, alidadavua Mhe. Siakalenge.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Utalii - Zambia Bw. Evans Muhanga alisema kuwa licha ya wasilisho zuri lilionesha ongezeko la watalii na mapato kwa Taifa, pia wamejionea watalii wengi katika maeneo mbalimbali ya vivutio walivyotembelea leo ikiwemo utalii wa puto ambapo zaidi ya puto 6 zilionekana zikielea angani zikiwa zimejaza watalii.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ismail Omary ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti alisema kuwa Ujumbe huo Maalumu kutoka serikali ya Zambia umeridhishwa na mikakati na mbinu mbalimbali za uhifadhi na utalii tulizoziwasilisha kwao zilizopelekea hifadhi hiyo kunyakua tuzo mbalimbali za kimataifa.

Aidha, Kamishna Ismail aliongeza kuwa hifadhi hiyo inajivunia kuwa na wanyama wakubwa watano (The Big 5) ikihusisha tembo, nyati, faru, simba na chui huku akisisitiza kuwa kwa mwaka 1993 hifadhi hiyo ilikuwa na faru weusi watatu tu lakini hadi 2025 hifadhi hiyo inajivunia kuwa na faru weusi zaidi ya 100.

Kabla ya wasilisho hilo, wajumbe hao  maalumu kutoka serikali ya Zambia walifanya utalii wa puto asubuhi na kujionea wanyama kutokea juu baadae walizuru maeneo mengine ya vivutio vya utalii likiwemo eneo la ndutu walipo nyumbu kwa sasa na kujionea nyumbu wakiwa na ndama lukuki.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...