Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya, inaendelea kujidhatiti kwa kuimarisha mifumo ya huduma za afya kupitia tafiti mbalimbali ili kuhakikisha wagonjwa wenye magonjwa adimu wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo Machi 4, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe wakati akifungua Kongamano la 16 la kusambaza matokeo ya tafiti za magonjwa adimu lililofanyika Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) jijini Dar es Salaam.

"Serikali inayapa uzito stahiki magonjwa haya adimu, ili tuweze kuyashughulikia kwa kina na upana wake, kwa kushirikiana na Taasisi kama Ali Kimara, sekta mashirika na sekta binafsi tutawafikia watoto wengi zaidi," amesema Dkt. Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe amesema hadi kufikia Desemba mwaka 2025 zaidi ya wataalamu wa afya 200 katika vituo 14 walikuwa wamepatiwa mafunzo ya kuanzisha vitengo vya tiba ya magonjwa adimu ikiwemo 'hemofilia' kuanzia ngazi ya msingi.

"Serikali imeshachukua hatua za kujenga uwezo wa maabara yetu ya Taifa, mafunzo kwa wataalamu wa Afya na kuanzisha vitengo maalum vya matibabu ya magonjwa adimu kuanzia ngazi ya msingi (Zahanati, kituo cha afya na hospitali za wilaya), tulianza na Seli mundu (Sickle cell) na sasa Hemofilia ambapo tayari wagonjwa 500 wamegundulika na wanaendelea na tiba,” amesema Dkt. Magembe.

Pia, katika Kongamano hilo Dkt. Magembe amewataka wataalamu hao wa tafiti wakiwemo MUHAS na NIMR kujadilina kwa kina na kwa uwazi kujua mafaniko, changamoto na kutoa mapendekezo na kuyawasilisha Serikalini yaweze kufanyiwa kazi.

Kongamano hilo limeandaliwa na Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ali Kimara Rare Disease Foundation (AKRDF).





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...