Na Munir Shemweta, WANMM

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameutumia uzinduzi wa “Samia Ardhi Kliniki” jijini Dar es Salaam kutangaza msimamo mkali wa Wizara dhidi ya vitendo vya uzembe na ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.

 

Katika hafla hiyo, Waziri Akwilapo amesema Wizara imeamua “kujivua gamba” na kuanza ukurasa mpya wa uwajibikaji, akisisitiza kuwa kauli za watumishi kudai mafaili kupotea au kutoonekana hazitavumiliwa tena.

 

“Hakuna kitu kama faili kupotea. Ofisi zetu zina mifumo thabiti, na mafaili hayana miguu ya kutoroka. Kauli hizi nimezipiga marufuku rasmi,” alisisitiza.

 

Waziri huyo alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi yanayolenga kurejesha imani ya wananchi kwa sekta ya ardhi, ambayo imekuwa ikikabiliwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu urasimu na usumbufu usio wa lazima.

 

Alisema Wizara haitasita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kukwamisha huduma kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa ardhi ni rasilimali ya Taifa na watumishi ni wasimamizi tu, si wamiliki.

 

Uzinduzi wa “Samia Ardhi Kliniki” umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kliniki hiyo itafanyika nchi nzima kuanzia Machi 2 hadi 7, 2026, ikitoa huduma za msaada wa kisheria, utoaji wa hatimiliki na elimu ya taratibu za umilikishwaji wa ardhi.

 

Mbali na kuhimiza wanawake kujitokeza kunufaika na huduma hizo, Waziri Akwilapo aliwataka wanaume na viongozi wa kaya kuachana na mila potofu zinazowanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi.

 

Kwa mujibu wa Waziri, idadi ya wanawake wenye hatimiliki imeongezeka hadi wastani wa asilimia 28 kutoka chini ya asilimia 10 miaka ya nyuma, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita.

 

Kauli mbiu ya zoezi hilo ni: “Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi Sasa,” ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw Edward Mpogolo akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila mbali na kuipongeza Wizara ya Ardhi kwa kuanzisha Samia Ardhi Kliniki amesema, kuna baadhi ya changamoto zilizoanza kujitokeza kwa wale wanaopata hati miliki za ardhi kufunga barabara zinazotumika kwa jamii.

 

Ameomba utaratibu wa fomu za kuthibitishwa na majirani katika maeneo yaliyorasimishwa kuzingaitiwa kwa kupitishwa katika ngazi husika na kusimamiwa ili kuepuka changamoto kama hizo.

 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemnera amesema huduma kubwa zinazotolewa kupitia Samia Ardhi Kliniki ni elimu hususan ya haki za umiliki kwa wanawake, ushauri wa mambo mbalimbali ya sekta ya ardhi, utoaji hati kwa waliokamilisha taratibu pamoja na huduma nyingine. 



 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa Kuzindua Samia Ardhi Kliniki jijini Dar es Salaam tarehe 2 Machi 2026
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi hati milki ya ardhi mmoja wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakati wa Samia Ardhi Kliniki tarehe 2 Machi 2026.
Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera akimkabidhi hati Miliki ya Ardhi Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Edrward Mpogolo katika tukio la uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki jijini Dar es Salaam tarehe 2 Machi 2026. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Dkt Upendo Matotola.
Sehemu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakipata huduma kupitia Samia Ardhi Kliniki inayoendelea jijini Dar es Salaam
Sehemu ya watumishi wa sekta ya ardhi wanawake wakitoa huduma katika Samia Ardhi Kliniki inayofanyika jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Upendo Matotola akimkabidhi mwanamama mkazi wa jiji la Dar es Salaam  Hati Milki ya ardhi katika Samia Ardhi Kliniki inayoendelea jijini Dar es Salaam.Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Lucy Kabyemera 
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MASSAKA, MICHUZI TV)





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...