Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo amesema kwamba madini ni muhimu si tu kwa rasilimali za kiuchumi bali pia ni nyenzo ya kuleta mabadiliko ya kweli katika maendeleo ya Afrika. 

Hivyo ametoa mwito kwa nchi za Afrika kushirikiana, kuweka sera madhubuti, na kuwekeza katika sekta ya madini ili kuhakikisha manufaa yake yanawafikia wananchi wote.

Singo ameyasema hayo leo  Aprili 27, 2026, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia wakati wa mkutano wa Jukwaa la Kikanda lililoandaliwa na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI.

Kauli mbiu katika jukwaa hilo inasema  “Kuchangamkia Madini Muhimu ya Afrika kwa Ajili ya Ujenzi wa Viwanda Kijani na Maendeleo Endelevu.” 

Singo katika hutuba yake iliyoangazia nafasi ya Afrika katika mustakabali wa uchumi wa dunia unaozingatia nishati safi, amesisitiza nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana, kuweka sera madhubuti na kuwekeza katika sekta ya madini ili manufaa yake yanawafikia wananchi wote

“Jukwaa hili limeweka msingi muhimu wa mijadala itakayochochea hatua za vitendo, huku likisisitiza kuwa mustakabali wa Afrika uko mikononi mwa Waafrika wenyewe, kupitia uongozi bora, ushirikiano, na matumizi sahihi ya rasilimali zake.”

Pia umuhimu wa kuwekeza katika uchakataji wa madini ndani ya nchi, ili kuongeza thamani, kuunda ajira, na kukuza uchumi wa viwanda huku akieleza tafiti zinaonyesha uwekezaji katika sekta hiyo unaweza kuongeza hadi dola bilioni 24 katika pato la taifa kwa mwaka na kuunda zaidi ya ajira milioni 2.3.

“Afrika inaongozwa na sera kama Africa Mining Vision na African Green Minerals Strategy, ambazo zinalenga kuimarisha viwanda, kuongeza thamani ya madini, na kuhakikisha maendeleo jumuishi. Pia, juhudi za kuanzisha minyororo ya thamani ya kikanda, kama ule wa betri na magari ya umeme unaoanzia Kongo na Zambia, zinaonyesha dhamira ya bara kujenga uchumi shindani.”

Amesema kupitia  mikakati ya pamoja na mifumo kama Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), bara linaweza kubadilisha utajiri wake wa madini kuwa chanzo cha ustawi endelevu huku akisema Afrika inakadiriwa kumiliki karibu asilimia 30 ya hifadhi ya madini muhimu duniani.

Baadhi ya madini hayo cobalt, lithium, graphite na madini adimu (rare earth elements). Kwa mfano, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huzalisha zaidi ya asilimia 70 ya cobalt duniani, huku nchi kama Zimbabwe, Mali, Tanzania na Msumbiji zikiwa na akiba kubwa ya lithium na graphite.

“Mahitaji ya madini haya yanatarajiwa kuongezeka kwa kasi ifikapo mwaka 2050, hasa kutokana na mabadiliko ya dunia kuelekea nishati safi. Hii inaipa Afrika fursa ya kipekee ya kukuza uchumi wake kupitia viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali zake.”

Kuhusu changamoto ya uongezaji thamani amesema licha ya utajiri huo, sehemu kubwa ya madini ya Afrika husafirishwa nje yakiwa ghafi, hali inayopunguza manufaa ya kiuchumi kwa nchi husika. Inakadiriwa kuwa ni takribani asilimia 2 tu ya biashara ya madini hufanyika ndani ya bara la Afrika.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, ameonya kuwa Afrika iko katika hatari ya kubaki maskini ikiwa itaendelea kuuza nje madini ghafi badala ya kuendeleza viwanda vya kuyachakata ndani ya nchi.

Amesisitiza bara hilo linaweza kukosa kunufaika na uchumi unaokua kwa kasi wa nishati safi licha ya utajiri wake mkubwa wa madini.Afrika ina akiba kubwa ya rasilimali muhimu kama vile cobalt, lithium, shaba na manganizi—madini muhimu kwa magari ya umeme, betri na mifumo ya nishati jadidifu.

Hata hivyo, madini mengi husafirishwa nje yakiwa ghafi, jambo linalopunguza ajira, ujuzi na ukuaji wa viwanda. Dessalegn alionya kuwa mpito wa nishati duniani unaweza kurudia mifumo ya kihistoria ambapo Afrika husambaza malighafi huku utajiri ukizalishwa kwingineko.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...