Benki ya Exim Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Toyota wenye lengo la kufanya umiliki wa magari kuwa rahisi zaidi na nafuu kwa Watanzania.

Kupitia ushirikiano huu, suluhisho maalum la ufadhili wa magari limeanzishwa, likiwwawezesha watu binafsi na biashara kununua magari mapya na yaliyotumika kwa gharama ndogo ya awali Pamoja na muda nafuu wa marejesho unaoweza kufikia hadi miaka sita.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji Saini huo, Mkuu wa Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi na wa Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Benki kuendelea kutoa suluhisho bunifu na zinazomlenga mteja moja kwa moja.

“Katika Benki ya Exim Tanzania, tunalenga kufanya zaidi ya huduma za Kibenki za kawaida kwa kutoa suluhisho zinazogusa mahitaji halisi ya kila siku ya wateja wetu. Ushirikiano huu na Toyota unatupa fursa ya kurahisisha umiliki wa magari kupitia mipango nafuu ya ufadhili inayopunguza mzigo wa kifedha huku ikiunga mkono mahitaji ya usafiri binafsi na ukuaji wa biashara,” alisema Lyimo.

Kupitia mpango huu, Benki ya Exim itatoa ufadhili wa hadi asilimia 80 ya gharama kwa magari mapya na asilimia 70 kwa magari yaliyotumika, kwa viwango vya riba shindani vinavyokokotolewa kwa mfumo wa salio linalopungua. Huduma hii inapatikana kwa Shilingi za Kitanzania na Dola za Marekani, ikiwa na malipo ya awali kuanzia asilimia 20.

Kifurushi hiki cha ufadhili wa magari kimetengenezwa ili kuwahudumia wateja mbalimbali wakiwemo waajiriwa, wajasiriamali, biashara ndogo na za kati (SMEs), pamoja na makampuni yanayohitaji suluhisho la uhakika la usafiri bila kuathiri mtiririko wa fedha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Toyota, Meneja Mkuu William Kadiva, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kupanua upatikanaji wa magari yenye ubora nchini Tanzania.

“Ushirikiano wetu na Benki ya Exim Tanzania ni hatua muhimu katika kuhakikisha magari ya Toyota yanawafikia Watanzania wengi zaidi. Kwa kuunganisha ubora wa magari yetu na suluhisho nafuu za ufadhili, tunawezesha watu wengi zaidi kumiliki magari yanayotegemewa kwa matumizi ya kila siku na shughuli za kibiashara,” alisema Kadiva.

Wateja wanaweza kupata huduma hii kwa kutembelea tawi lolote la Exim Bank au showroom za Toyota (Automark) kote nchini ili kujionea chaguo zilizopo na kuanza safari ya kumiliki gari.

Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya Exim Bank na Toyota ya kuchochea shughuli za kiuchumi, kuboresha usafiri, na kuunga mkono ukuaji wa biashara nchini Tanzania.

Kuhusu Exim Bank Tanzania

Ilianzishwa mwaka 1997, Exim Bank Tanzania ni mojawapo ya taasisi zinazoongoza za kifedha nchini, inayotambulika kwa ubunifu wake, suluhisho zinazomlenga mteja, na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Ikiwa na uwepo imara wa kikanda katika nchi za Comoro, Djibouti, Uganda, na Ethiopia, Exim Bank ni miongoni mwa benki chache za asili ya Tanzania zilizofanikiwa kupanua shughuli zake nje ya mipaka ya nchi.

Kupitia mtandao wake mpana wa matawi na majukwaa ya kisasa ya huduma za benki kidijitali, Exim Bank inaendelea kuwawezesha watu binafsi na biashara kwa huduma za kifedha zilizo thabiti, rahisi kubadilika, na zenye mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.


Kuhusu Toyota Tanzania

Toyota Tanzania Ltd, iliyoanzishwa mwaka 1965, ni msambazaji pekee wa magari ya Toyota nchini Tanzania na mdau mkuu katika sekta ya magari. Kampuni hii hutoa aina mbalimbali za magari na huduma. Imeendelea kushikilia nafasi ya uongozi katika soko la magari mapya nchini, kwa kuzingatia uendelevu na kutoa suluhisho bora za usafiri kwa wateja wake.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na wa Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Bw.Andrew Lyimo( wa pili kushoto) na Meneja Mkuu wa Toyota Tanzania Bw.William Kadiva (wa pili kulia) wakisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano unaolenga kuwawezesha wateja wake kumiliki gari ya ndoto yake. Hafla hii ilifanyika ofisi za Toyota Tanzania, jijini Dar es Salaam tarehe 21 April 2026, Ikishuhudiwa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Bw. Stanley Kafu (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Sheria wa Toyota Tanzania Bi. Lucia Minde (kulia).

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...