Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma 

Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, ameishauri Serikali kuweka historia mpya kwa kutunga sheria maalum itakayolinda miundombinu ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miradi ya maendeleo unadumu kwa muda mrefu na kuwa na tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni mjini Dodoma, Bulaya amemuomba Waziri Mkuu  Dkt Mwigulu Nchemba, kuchukua hatua madhubuti kwa kuanzisha mfumo wa kisheria utakaolinda barabara, madaraja pamoja na miradi mingine mikubwa ya kimkakati.

Bulaya alisisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Taifa kuweka utamaduni wa kutenga fedha mahsusi kwa ajili ya matengenezo na ulinzi wa miundombinu, badala ya kusubiri miradi iharibike ndipo hatua zichukuliwe. Alibainisha kuwa mara nyingi Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kujenga miradi mipya, lakini juhudi za kuitunza na kuilinda zimekuwa hazipewi uzito unaostahili.

“Lazima kama Taifa, kwenye dira yetu ya maendeleo, tuanze kuwa na utamaduni wa kuweka fedha za kulinda miradi ya nchi hii. Hii itasaidia kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unadumu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu,” alisema Bulaya.

Aidha, mbunge huyo alieleza kuwa kasi ya maendeleo inayoshuhudiwa nchini chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan, inapaswa kuambatana na mikakati thabiti ya kuhakikisha ubora wa miradi hiyo unadumishwa. Alionya kuwa bila kuwepo kwa mfumo madhubuti wa ulinzi na matengenezo, baadhi ya miradi inaweza kupoteza thamani yake mapema na hivyo kuisababishia nchi hasara.

Bulaya alisisitiza pia dhana ya “kupanga ni kuchagua”, akihimiza Serikali kuweka vipaumbele vinavyolenga kulinda uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya miundombinu. Kwa mujibu wake, ni bora kutumia rasilimali kidogo kulinda kilichopo kuliko kutumia fedha nyingi kujenga upya miradi iliyoharibika.

Katika hatua nyingine, alionya kuwa iwapo hoja hiyo haitapatiwa majibu ya kuridhisha na Serikali, yuko tayari kuchukua hatua zaidi za kibunge ili kuhakikisha suala la ulinzi wa miundombinu linapewa uzito unaostahili.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...