Viongozi wa vyama vya ushirika mkoani Geita wametakiwa kusimamia maadili kwa dhati ili kuhakikisha wadau, hususan wakulima wadogo, wanapata haki na stahiki zao kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, wakati wa kilele cha Jukwaa la 4 la Maendeleo ya Ushirika mkoani humo lililofanyika Aprili 22 mwaka huu.
Katika hotuba yake, Mhe. Komba amezitaka AMCOS mbalimbali kuhakikisha zinawalipa wadau madeni yao kila msimu unapoisha. Alibainisha kuwa kwa sasa halmashauri pekee zinadai takribani Shilingi Milioni 50 huku wanunuzi wakidai takribani Shilingi Milioni 100, hali ambayo alionya kuwa inaweza kuhatarisha uhakika wa soko la mazao na bidhaa mbalimbali mkoani humo ikiwa hatua hazitachukuliwa.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Geita, Bi. Doreen Mwanry, amewahimiza wananchi ambao bado si wanachama kujiunga na ushirika ili kupata huduma sahihi.
Alieleza kuwa mkoa una jumla ya vyama 629 vyenye wanachama 5,084, na tayari vyama hai 304 vimeshasajiliwa kwenye Mfumo wa kusajili na kusimamia vyama vya ushirika nchini (MUVU).
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Elfas Msenya, ametoa wito kwa AMCOS kusimamia taratibu za mfumo wa stakabadhi ya ghala kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye zao la dengu msimu uliopita.
Alisisitiza kuwa kufuata taratibu hizo kutawezesha mazao yote kuingizwa kwenye mfumo na kuhakikisha wakulima wanapata faida kulingana na bei elekezi zilizotangazwa.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...