Wananchi na Wamiliki wa Ardhi Mkoani Kagera wametakiwa kulupia Kodi ya Ardhi kwa wakati ili kuepuka Usumbufu na Migogoro inayoweza kujitokeza.

Wito huu umetolewa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kagera, Ndugu Erick Peter Makundi, kwa wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka malimbikizo pamoja na usumbufu unaoweza kujitokeza baadaye, na kusisitiza kuwa ulipaji wa kodi hiyo si hiari, bali ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi, na unachangia moja kwa moja katika kuboresha huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Aprili 29 mwaka huu, Makundi ameeleza kuwa Serikali imeweka sheria madhubuti kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi. 

Hata hivyo amebainisha kuwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kufutiwa hati za umiliki wa ardhi au hata kuchukuliwa hatua za kisheria mahakamani. Hivyo, kuwataka wananchi kutekeleza wajibu wao kwa hiari ili kuepuka madhara hayo.

Kwa upande mwingine, Makundi alifafanua kuwa iwapo wananchi wote wanaodaiwa watalipa kodi hiyo kwa wakati, zaidi ya shilingi bilion 20 zinaweza kukusanywa, jambo litakaloongeza mapato ya serikali na kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Pia alitaja baadhi ya changamoto wanazoweza kukutana nazo wadaiwa, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutumia hati zao za ardhi kupata mikopo au kuzitumia kama dhamana hadi watakapomaliza kulipa madeni yao.

Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kutoa maoni yao wamesema kuwa wamepokea wito huo kwa mtazamo chanya, huku wakieleza kuwa wako tayari kutimiza wajibu wao kwa kulipa kodi kwa wakati huku wakiiomba  serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusu umuhimu wa kodi ya ardhi pamoja na kuboresha mifumo ya ulipaji ili iwe rafiki na rahisi kwa kila mwananchi kuitumia bila changamoto.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...