Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Wataalamu wa afya na mazingira wameendelea kuonesha wasiwasi juu ya kuenea kwa magonjwa ya malaria na kichocho barani Afrika, wakieleza kuwa bado ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya zinazoathiri maendeleo ya jamii hasa kutokana na kushamiri kwa kilimo cha mpunga kwenye maeneo mengi na kuongeza mazalia ya Mbu na konokono wamaoneza magonjwa hayo.

Mtafiti kutoka Shule ya London ya Usafi wa Afya na Tiba ya Magonjwa ya Tropiki Dkt. Laura Braun wakati wakifanya wasilisho lake kuhusu kilimo cha Mpunga kinavyochangia mazalia ya konokono wanaoeneza ugonjwa kichocho.
Hayo yamesemwa na wataafiti kutoka Shule ya London ya Usafi wa Afya na Tiba ya Magonjwa ya Tropiki Prof. Jo Lines na Dkt. Laura Braun wakati wakifanya wasilisho lao mbele ya watafiti wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) pamoja na Watafiti wa Kituo cha Kusini mwa Afrika cha Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kuambukiza (SACIDS) kuhusu mahusiano ya magonjwa hayo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuangalia namna ya kuongeza ushirikiano na kubuni njia za pamoja za kukabiliana na kuenezwa kwa magonjwa hayo nchini Tanzania.
Akifanya wasilisho lake Prof. Jo Lines alieleza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika, ugonjwa wa malaria bado unaathiri kwa kiwango kikubwa bara la Afrika, na hivyo kuhitaji mikakati madhubuti zaidi ya kudhibiti na hatimaye kuutokomeza.
“Afrika inabeba zaidi ya asilimia 85 ya mzigo wa malaria duniani lakini pia unaendelea kusababisha vifo kila dakika, hali inayodhihirisha uzito wa tatizo hili na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na shirikishi katika kupambana nao kwani mbu aina ya Anopheles gambiae ndiye msambazaji hatari zaidi wa malaria barani Afrika nah ii ni kwa sababu mbu huyu ana uwezo mkubwa wa kusambaza vimelea vya ugonjwa huo kwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na aina nyingine za mbu wanaopatikana katika maeneo mengine duniani” alifafanua Prof. Lines.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza kuwa udhibiti wa mbu hawa unapaswa kupewa kipaumbele kwa kutumia mbinu jumuishi huku akipendekeza matumizi ya vyandarua vyenye dawa, kunyunyizia viuatilifu, pamoja na kuboresha mazingira ili kupunguza mazalia ya mbu, hususan katika maeneo yenye maji yaliyotuama.
Katika hatua nyingine, Prof. Jo Lines aliangazia uhusiano uliopo kati ya malaria na kilimo cha mpunga na kusema kuwa zao la mpunga linaendelea kukua kwa kasi barani Afrika na hasa katika maeneo ya karibu na miji, jambo ambalo linaongeza uzalishaji wa chakula lakini pia linaibua changamoto mpya za kiafya.
Aidha alifafanua kuwa mashamba ya mpunga yanaweza kuwa mazalia mazuri ya mbu kutokana na uwepo wa maji ya kudumu na muda mfupi hali hii inaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya malaria endapo hatua stahiki za udhibiti hazitachukuliwa.
Akizungumzia ugonjwa wa Kichocho (schistosomiasis) Dkt. Laura Braun alieleza kuwa ugonjwa huo unaendelea kuwa tishio kubwa la afya ya jamii, hasa katika maeneo yenye vyanzo vya maji yasiyo salama na kubainisha kuwa ugonjwa huo husababishwa na minyoo aina ya Schistosoma na unaathiri zaidi ya watu milioni 240 duniani.
Dkt. Braun alifafanua kuwa maambukizi ya ugonjwa huo hutokea pale mtu anapogusana na maji yenye konokono walioambukizwa ambao hubeba vimelea vinavyoweza kupenya moja kwa moja kupitia ngozi ya binadamu na kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo upungufu wa damu na uharibifu wa viungo vya ndani.
“Mazingira ya kilimo cha mpunga yanaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya kichocho kwani maji ya kina kifupi, yenye joto na yasiyotembea kwa kasi huwa mazuri kwa kuzaliana kwa konokono wanaobeba vimelea hivyo na kutokana na hali hiyo wakulima wa mpunga huwa katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa kutokana na kukaa muda mrefu ndani ya maji wakati wa shughuli za kilimo” alibainisha Dkt. Braun.
Mtafiti huyo amesisitiza umuhimu wa wakulima kuchukua hatua za kinga, ikiwa ni pamoja na kuvaa vifaa vya kujikinga kama buti, kuboresha usimamizi wa maji mashambani, na kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia za maambukizi.
Sambamba na hilo alieleza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya afya na kilimo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa uzalishaji wa chakula unaenda sambamba na ulinzi wa afya za wananchi kwa kufanya kilimo rafiki kwa binadamu na kinachozuia kuzaliana kwa konokono hao pamoja na mbu hao wanaoeneza ugonjwa wa Maralia.
Awali akizungumzia lengo la ziara hiyo ya watafiti nchini Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) Prof. Suzana Nchimbi Msolla amesema watafiti hao wanatafuta njia rafiki ambayo inaweza kutumika kwenye mashamba hayo ya mpunga kuzuia kuzaliana kwa vimelea vya magonjwa hayo kwa kufuga samaki na bata ambao watakula mayai na vuluilui vya Mbu na Konokono na kupunguza kuzaliana na kutunza afya ya binadamu pamoja na kuongeza kipato kwa wakulima.
“Wamekuja baada ya kuona kuwa sisi kama mradi tunafanya utafiti kwenye zao la mpunga kwa muda mrefu hivyo wakataka kutushirikisha kuhusu utafiti wao na kujadiliana kuona uwezekano wa matumizi ya njia wanazopendekeza kama zitafaa kwa mazingira ya Tanzania hasa baada ya kuona kuwa njia kama hizo zimeweza kufanya kazi kwenye nchi zingine kama vile China,Mashariki kwa ulaya na Asia ya kati” Alieleza Prof. Msolla.
Prof. Msolla amesema wataalamu bado wanasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kinga kama vile kuvaa vifaa vya kujikinga (boots), kuboresha usimamizi wa maji mashambani, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia za maambukizi kwani hatua hizp zinaweza kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za ugonjwa huu katika jamii zinazotegemea kilimo cha mpunga.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kusini mwa Afrika cha Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kuambukiza (SACIDS) Prof. Gerald Misinzo akieleza uzoefu wake kwenye magonjwa ya kuambukiza kupitia mbinu ya Afya moja.

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) Prof. Suzana Nchimbi Msolla akifafanua jambo kwa kutoa uzoefu wake kwenye tafiti za zao la mpunga nchini.

Mtafiti Mbobevu kwenye Ufugaji wa viumbe maji kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama na Viumbebaji ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Renalda Mnubi akieleza jambo wakati wa mjadala huo.

Mtafiti kutoka Shule ya London ya Usafi wa Afya na Tiba ya Magonjwa ya Tropiki Prof. Jo Lines akieleza mahusiano ya Kilimo cha Mpunga na kueneo kwa ugonjwa maralia afrika na dunaini na namna ya kukabiliana nao.

Watafiti hao wakichua sampuli kwaajili ya kupeleka maabara za SUA kuangalia uwepo wa vimelea kwenye eneo la shamba la majaribio ya kilimo cha mpunga.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...