Na Farida Mangube Morogoro

Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu imewatoa hofu wakazi wa Manispaa ya Morogoro kuwa maji ya Bwawa la Mindu ni salama, kwani kemikali iliyomwagika haikufikia chanzo cha maji.

Wasiwasi huo ulizuka kufuatia ajali ya lori lililokuwa likisafirisha kemikali aina ya sulphur kuacha njia na kugonga miti mita 300 kutoka bwawa la Mindu mtaa wa mikoroshini Kata ya Mindu barabara kuu ya Morogoro–Iringa.

Mkurugenzi wa Bonde la Maji bonde la Wami-Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi, amesema hatua za haraka zilizochukuliwa na wataalamu zilisaidia kuzuia kemikali hiyo kusambaa hadi kwenye chanzo cha maji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), CPA Sais Kyejo, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa hakuna madhara yaliyobainika katika ubora wa maji yanayosambazwa.

“Wananchi waendelee kutumia maji bila hofu,” amesema Kyejo.

Naye Meneja wa Kanda ya Kati wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bi Magdalena Mtenga, amesema hadi sasa hakuna madhara yaliyoripotiwa kwa wananchi, licha ya kemikali hiyo kuwa hatarishi endapo itashughulikiwa bila tahadhari.

Ameeleza kuwa sulphur ina sifa ya kuwaka na hata kulipuka, pamoja na kusababisha muwasho wa ngozi au koo, lakini hali hiyo haikutokea wakati wa operesheni ya kuiondoa katika eneo la ajali.

Taasisi mbalimbali zikiwemo Bonde la Wami-Ruvu, MORUWASA, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zilishiriki kuondoa kemikali hiyo kwa usalama.

Meneja wa NEMC Kanda ya Morogoro na Rufiji, Arnold Mapinduzi, amesema kemikali hiyo itateketezwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda mazingira.

Ajali hiyo ni ya tatu ndani ya mwezi mmoja kuhusisha usafirishaji wa kemikali aina ya sulphur Barabara kuu ya Morogoro - Iringa hali inayochochea haja ya kuimarisha usalama wa usafirishaji wa kemikali hatarishi.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...