Pamela Mollel Arusha.
Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Nicas Mawazo, amejitosa katika kinyang’anyiro cha uongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania, huku akiahidi kuleta mageuzi yatakayoiimarisha taasisi hiyo katika kusimamia maendeleo ya serikali za mitaa nchini.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika kesho, Aprili 22, 2026, katika Arusha International Conference Centre, ambapo Dk Mawazo anawania nafasi ya uenyekiti inayoshikiliwa kwa sasa na Murshid Hashim Ngese.
Katika kinyang’anyiro hicho, Dk Mawazo anatarajiwa kuchuana na wagombea wengine akiwemo Sima Constantine Sima pamoja na Maximilian Iranghe.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 21, 2026, mara baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa, Dk Mawazo amesema dhamira yake ni kuifanya ALAT kuwa chombo imara zaidi kitakachowezesha utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Nimekuja kurejesha fomu ya uchaguzi wa ALAT ili kuomba ridhaa ya kuongoza taasisi hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa akichaguliwa, atahakikisha ALAT inaimarika zaidi ili iwe sauti ya wananchi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya, barabara na huduma nyingine za kijamii.
“Sisi ndio tunaoletewa fedha na kuzielekeza kwenye miradi ya wananchi kama hospitali, shule na miundombinu ya barabara,” amesema.
Aidha, Dk Mawazo amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na ALAT, bado kuna haja ya kuimarisha mifumo ya uendeshaji ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya kwa jamii.
“ALAT ina mafanikio, lakini nikipata nafasi nitaleta mabadiliko makubwa kutokana na uzoefu wangu wa uongozi. Ninaamini naweza kuongoza taasisi hii kwa ufanisi zaidi,” ameongeza.
Mkutano huo wa uchaguzi utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT, Thomas Vungwa, mkutano huo wa siku mbili utahusisha uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Amesema wajumbe kutoka halmashauri 184 nchini wanatarajiwa kushiriki, huku mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulioanza Aprili 17, 2026 ukifikia tamati sambamba na kuanza kwa uchaguzi huo kesho.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...