
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Jiji
la Dar es Salaam linatarajia kuandika historia mpya katika tasnia ya
burudani baada ya kutangazwa kwa uzinduzi wa tamasha la kwanza la
kimataifa la vichekesho, Punchline International Comedy Festival (PICF)
2026, litakalofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026.
Tamasha
hilo lililotangazwa na Punchline Africa, linatarajiwa kuwakutanisha
wachekeshaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa kipindi cha wiki moja,
likijumuisha maonesho ya jukwaani, shughuli za vyombo vya habari pamoja
na ubadilishanaji wa utamaduni. Kilele cha tamasha hilo kitakuwa Grand
Finale itakayofanyika katika ukumbi wa The Superdome.
PICF
2026 itahusisha maonesho ya vichekesho kwa lugha ya Kiswahili na
Kiingereza, hatua inayolenga kuonesha utofauti wa vipaji vya wacheshi
barani Afrika. Waandaaji wamesema mbali na burudani, tamasha hilo lina
lengo la kuhamasisha umuhimu wa vichekesho katika kuboresha afya ya
akili kwa kuwapa watu nafasi ya kucheka, kupunguza msongo wa mawazo na
kuunganishwa kijamii.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Mwanzilishi Mwenza wa Punchline Africa, Evans
Bukuku, alisema tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuleta watu pamoja na
kuwapa nafuu ya kihisia kupitia sanaa ya uchekeshaji.
“Comedy
siyo kuchekesha tu, ni njia ya kuelewa maisha na kupunguza msongo wa
mawazo. Kupitia PICF tunataka watu waondoke wakiwa na nafuu hata kama
changamoto bado zipo,” alisema.
“Comedy
siyo kuchekesha tu, ni njia ya kuelewa maisha na kupunguza msongo wa
mawazo. Kupitia PICF tunataka watu waondoke wakiwa na nafuu hata kama
changamoto bado zipo,” alisema.Kwa
upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini, Anne Sophie Ave, alisema
wameamua kuunga mkono tamasha hilo kutokana na mchango wa sanaa katika
kukuza vipaji vya vijana na kuwajengea kujiamini.
Aliongeza
kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake kama
kitovu cha Afrika Mashariki na historia yake katika harakati za
Pan-Afrika, akisisitiza kuwa sanaa ya vichekesho inaweza kuwa daraja la
kuunganisha bara hilo.
Naye
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu nchini, Emmanuel Ndumukwa, alisema
serikali inaunga mkono juhudi hizo na kuona kuwa tamasha hilo linaweza
kuwa chachu ya kukuza tasnia ya uchekeshaji nchini.
Kwa
upande wa wasanii, mchekeshaji Humphrey Richard alisema PICF 2026 ni
fursa adhimu kwa wacheshi kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufikia
masoko ya kimataifa.
Tamasha
hilo linaandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Alliance
Française Dar es Salaam, Tanzania Film Board pamoja na SGA Security.
Aidha,
PICF ni sehemu ya mradi wa Création Africa unaofadhiliwa na Ubalozi wa
Ufaransa, unaolenga kuwawezesha wasanii na taasisi za ubunifu nchini.
Tamasha
hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki na kufikia zaidi ya watu
milioni moja kupitia majukwaa ya kidigitali, huku taarifa za wasanii
watakaoshiriki na ratiba kamili zikitolewa katika siku zijazo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...