Na Mwandishi wetu -Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza rasmi kufanyika kwa hafla ya nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026, akisisitiza kuwa tuzo hizo zimeendelea kuwa chachu muhimu ya kukuza fasihi ya Kiswahili na kuibua vipaji vya waandishi bunifu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Aprili 8, 2026, Prof. Mkenda amesema hafla hiyo itafanyika Aprili 13, 2026 katika ukumbi wa Super Dome, Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliyetoa mchango mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili na fasihi.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa tuzo hizo zimeendelea kuvutia washiriki wengi zaidi kila mwaka kutoka ndani na nje ya nchi. “Kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), inayoratibu tuzo hizo kwa kushirikiana na kamati huru inayoongozwa na Prof. Penina Mlama, mwaka huu washindani walijitokeza kwa wingi katika nyanja nne kuu: riwaya, hadithi za watoto, tamthilia na ushairi,” amesema Waziri Mkenda.
Hafla ya mwaka huu itapambwa na uwepo wa mgeni rasmi, mshairi mashuhuri duniani Abdilatif Abdalla kutoka Ujerumani, ambaye pia aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15, jambo linaloipa hafla hiyo uzito wa kipekee kitaifa na kimataifa.
Aidha, kabla ya hafla hiyo kutangazwa washindi, kutakuwa na mjadala maalum utakaowakutanisha waandishi bunifu wa ndani na nje ya nchi, ukiwahusisha wataalamu mashuhuri akiwemo Dkt. Aida Mutenyo kutoka Uganda na Ferdinand Ndahayo kutoka Rwanda.
Kuhusu mafanikio ya tuzo hizo, Prof. Mkenda amesema tangu kuanzishwa kwake, jumla ya Watanzania 27 wamefanikiwa kushinda katika makundi mbalimbali, huku Serikali ikiwekeza takribani shilingi milioni 800 kwa ajili ya uchapishaji wa vitabu vilivyoshinda na kusambazwa katika shule za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhamasisha utamaduni wa kusoma.
“Tuzo hizi pia zimekuwa zikivutia Watanzania waishio nje ya nchi pamoja na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, hali inayoonyesha kukua kwa hadhi ya tuzo hizi kimataifa,” amesema Prof. Mkenda, akishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza uwekaji wa mazingira wezeshi katika kukuza sekta ya fasihi na uandishi bunifu.
Waziri Mkenda pia ameipongeza kamati huru ya tuzo chini ya uongozi wa Prof. Penina Mlama kwa kusimamia mchakato wa upatikanaji wa washindi kwa weledi, haki na uwazi. Aidha, amewaalika wananchi kushiriki katika hafla hiyo itakayoanza saa nane mchana, ambapo mbali na kutangazwa kwa washindi, pia kutakuwa na burudani ya kazi za kibunifu pamoja na majadiliano yatakayochochea maendeleo ya fasihi nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu 2026, Prof. Penina Mlama, amesema mwitikio wa washiriki umekuwa mkubwa na unaonyesha kukua kwa tasnia ya uandishi bunifu. Washindi watatu bora kwa kila kipengele watapata zawadi ya fedha taslimu pamoja na fursa ya kuchapishiwa kazi zao.




.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...