Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma 

Serikali imesema imepokea rasmi ushauri wa wabunge kuhusu kuanzishwa kwa mfumo wa bima ya afya kwa wakulima, hususan wale wanaojihusisha na zao la korosho, huku ikiweka wazi kuwa tayari imeanza mchakato wa kufanya tathmini ya kina ili kubaini namna bora ya kutekeleza mpango huo.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma Aprili 29, 2026 wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa pendekezo hilo na inalipa uzito unaostahili kutokana na mchango mkubwa wa wakulima katika uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa hatua ya awali ni kufanya uchambuzi wa kina utakaosaidia kubaini muundo sahihi wa bima hiyo, ikiwemo gharama, walengwa, na namna ya kuisimamia ili iweze kuwa endelevu na yenye manufaa kwa wakulima.

“Hoja ya bima ya afya kwa wakulima wa korosho tumeipokea. Tunakwenda kufanya tathmini ya kina ili kujua namna bora ya kuitekeleza. Baada ya hapo, tutakaa na wadau mbalimbali kuona jinsi ya kuanzisha mpango huo kwa ufanisi,” alisema Chongolo.

Aidha, Waziri huyo amebainisha kuwa mpango huo hautalenga wakulima wa korosho pekee, bali Serikali inalenga kuupanua ili kuwahusisha wakulima wa mazao mengine ya kimkakati kama pamba, tumbaku na mazao mengine yanayolimwa kwa wingi nchini.

Chongolo amesema kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuboresha ustawi wa wakulima kwa kuwapatia kinga ya kiafya, jambo litakalowasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na hatimaye kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa nchi, pamoja na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata huduma bora za kijamii zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Wadau wa sekta ya kilimo wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wakulima, wakieleza kuwa changamoto za kiafya mara nyingi huathiri uzalishaji na kipato chao. Kupitia mpango huu unaopendekezwa, inatarajiwa kuwa wakulima watanufaika kwa kupata huduma za afya kwa gharama nafuu au kwa mfumo unaowawezesha kumudu kulipia huduma hizo kwa urahisi zaidi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...