Na Pamela Mollel,Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Riziki Shemdoe amesema taasisi ya mpango wa usalama barabarani (TARSI) ina mchango mkubwa katika kuimarisha taaluma ya uhandisi na kupunguza ajali za barabarani kupitia utoaji wa mafunzo kwa wataalamu nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wahandisi kuhusu usalama barabarani, Shemdoe alisisitiza kuwa serikali inaona umuhimu wa wahandisi kuendelea kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika ubunifu na usimamizi wa miundombinu salama.
Alieleza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuhakikisha barabara zinakuwa salama zaidi kwa watumiaji wote, ikiwa ni pamoja na madereva, waendesha pikipiki na watembea kwa miguu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Maliki Barongo, alisema taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu na tafiti zinazolenga kupunguza ajali za barabarani, huku akihimiza wadau kushirikiana kwa karibu ili kufikia malengo hayo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI), Dkt. Joel Bwemelo, alieleza umuhimu wa kuchukua tahadhari na kuzingatia kanuni za usalama barabarani ili kupunguza athari za ajali zinazoweza kuepukika.
Aidha, Laurent Maganga kutoka Norplan Tanzania alipendekeza elimu ya usalama barabarani iingizwe katika mitaala ya uhandisi, akisema hatua hiyo itasaidia kuzalisha wahandisi wenye uelewa mpana wa masuala ya usalama tangu wakiwa vyuoni.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wahandisi kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakilenga kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kitaalamu zitakazochangia kuboresha ubora wa barabara pamoja na kupunguza ajali zinazotokana na mapungufu ya miundombinu.



.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...