Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya Askari Polisi aitwaye Roland Mollel ambaye ni mkazi wa Arusha yaliyotokea Aprili 15, 2026 muda wa usiku.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa tukio hilo lilitokea huko katika mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet Jijini Arusha.
Kamanda Masejo amebainisha kuwa Askari huyo wakati akiendelea na shughuli zake binafsi baada ya kazi, kulitokea taharuki iliyotokana na kusambaa maneno ya kundi la watu wakidai katika eneo lao kuna wezi wameonekana.
Ameendelea kufafanua kuwa wakati hayo yakiendelea, marehemu akiwa anapita na mtu mwingine ambaye inadaiwa ni dereva bodaboda wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, kundi hilo lilianza kuwashambulia huku wakiwakimbiza.
Aidha, amebainisha kuwa wanaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao wamehusika na pia wanakamilusha uchunguzi wa tukio hilo.
Jeshi la Polisi mkoani humo limetoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaoendekeza tabia za kuchukua sheria mkononi kwa kuongozwa na mihemko kuacha kwani watambue wakifanya hivyo ni kuvunja sheria pamoja na kusababisha madhara kwa watu ambao hawana hatia.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...