Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, tarehe 9 Aprili 2026 amekutana na kufanya mazungumzo ya kikazi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guy Kabombo Muadiamvita, aliyekuwa katika ziara rasmi nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia wa ulinzi kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika kikao hicho, Dkt. Nyansaho alimhakikishia mgeni wake kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, iko tayari kuendeleza ushirikiano na DRC katika sekta mbalimbali za ulinzi. Maeneo hayo ni pamoja na kubadilishana wataalamu, kutoa mafunzo ya kijeshi, pamoja na kushirikiana kukabiliana na changamoto za kiusalama kama uhalifu wa mtandaoni na ugaidi.
Aidha, Dkt. Nyansaho alieleza kuwa ziara ya Mhe. Kabombo ni ishara ya uhusiano imara uliopo kati ya nchi hizo mbili, na inaonesha dhamira ya pamoja ya kuendeleza urafiki, maelewano na ushirikiano wa muda mrefu. Alisisitiza kuwa mazungumzo ya mara kwa mara yamekuwa msingi muhimu katika kujenga ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na DRC.
“Nina imani kuwa kupitia ushirikiano wetu, tutaweza si tu kukabiliana na changamoto za pamoja, bali pia kutumia fursa zilizopo kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wetu,” alisema Dkt. Nyansaho.
Kwa upande mwingine, alibainisha kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na DRC una nafasi kubwa ya kuimarika zaidi, hususan kupitia matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam katika usafirishaji wa mizigo, jambo litakalochochea maendeleo ya pande zote mbili.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...