Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), kama sehemu ya kurudisha kwa jamii, imetoa msaada katika kituo cha kulelea watoto cha Tupendane kilichopo jijini Dodoma huku ikitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwa na moyo wa kusaidia jamii, hususan vituo vya kulelea watoto.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Subira Yasini, mlezi wa Kituo cha Tupendane, ameishukuru TCAA kwa kuguswa na mahitaji ya kituo hicho na kueleza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha huduma na mazingira ya malezi kwa watoto waliopo kituoni. Alisema hatua hiyo inaonesha mshikamano na kujali ustawi wa makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.
Awali, Bi. Subira alieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa eneo la kudumu la makazi ya watoto hao, kwani kwa sasa wanatumia eneo la mtu aliyewapatia hifadhi ya muda.
Kituo hicho cha Tupendane kina jumla ya watoto 35, ambapo 22 kati yao wanasoma katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.
Kwa upande wake, Ally Changwila, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi, alisema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha mahusiano chanya na jamii kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii. Ameeleza kuwa msaada uliotolewa katika kituo hicho unaakisi dhamira ya TCAA ya kuchangia ustawi wa jamii sambamba na majukumu yake ya msingi katika usimamizi wa usafiri wa anga.
Aidha, aliongeza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA ameelekeza kuwa, kutokana na umuhimu wa kurejesha kwa jamii na kusaidia wenye uhitaji, kila robo ya mwaka wa fedha angalau TCAA itoe msaada katika mojawapo ya vituo vyake vya kazi nchini. TCAA ina vituo 16 nchi nzima vinavyotoa huduma ya uongozaji ndege.
Kwa upande wake, Aswile Kamendu, Meneja wa TCAA Kituo cha Dodoma, alisema kuwa TCAA itaendelea kushirikiana na Taasisi na vituo mbalimbali vya kijamii katika mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ili kusaidia juhudi za Serikali na wadau wengine katika kuboresha maisha ya wananchi.
Msaada uliotolewa katika kituo hicho cha Tupendane ni pamoja na vyakula vya aina mbalimbali, sabuni, mafuta ya kupikia pamoja na vifaa vya shule ikiwemo mabegi na madaftari.
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) Ally Changwila (wa pili kulia) aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi pamoja na Meneja wa TCAA Kituo cha Dodoma Aswile Kamendu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya walezi na watoto wanaolelewa katika kituo cha Tupendane kilichopo jijini Dodoma
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) Ally Changwila akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi wakati wa kutoa msaada katika kituo cha kulelea watoto cha Tupendane kilichopo jijini Dodoma
Meneja wa TCAA Kituo cha Dodoma Aswile Kamendu akizungumza kuhusu namna watakavyoendelea kushirikiana na Taasisi na vituo mbalimbali vya kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali katika mkoa wa Dodoma








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...