Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
JUMLA ya vijana na watoto 75,500 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa Selimundu katika mradi wa miaka mitatu unaotekelezwa nchini Tanzania na Kenya, hatua inayolenga kubaini mapema wenye tatizo hilo na kuwapatia huduma stahiki.
Katika mpango huo, watoto wachanga 45,000 watafikiwa, huku watoto wa chini ya miaka mitano wakiwa 12,500 na vijana 18,000 wakipangwa kunufaika na uchunguzi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Dkt. Gunini Kamba amesema bado kuna changamoto ya kuwabaini mapema watoto na vijana wenye selimundu hali inayochangia kuchelewa kwa huduma muhimu. Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuongeza ufanisi wa utambuzi wa mapema na matibabu.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wana vinasaba vya selimundu huku ugonjwa huo ukichangia vifo vya asilimia 5 hadi 7 kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wataalam Wanaopambana na Selimindu nchini Tanzania, Dkt. Elisha Osati, amesema mradi huo pia utalenga kuwafikia vijana ili wafahamu hali zao za vinasaba, akisisitiza kuwa hali hiyo haiwezi kujulikana bila kupimwa.
Amefafanua kuwa mtu hupata ugonjwa wa sikoseli pale anaporithi vinasaba viwili kutoka kwa wazazi wote wawili, hivyo elimu kwa vijana ni muhimu ili waweze kufanya maamuzi sahihi wanapoingia kwenye mahusiano.
Naye shujaa wa Selimundu, Samwel Maingu, amesema aligundulika kuwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 18, akihimiza jamii kujenga utamaduni wa kupima mapema ili kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Shujaa wa Selimundu, Samwel Maingu akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka mitatu wa Selimundu unaotekelezwa Tanzania na Kenya. Uzinduzi huo umefanyika leo Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...