Na Vero Ignatus
BENY Israel Mwaisaka, mchungaji wa kanisa la FPCT Komwale lililopo nje kidogo ya mji wa Handeni, wilaya ya Handeni mkoani Tanga anasema kuwa ninatambua na kuthamini Amani ambayo imekwepo tangu nchi ipate uhuru imekuwa msingi mkubwa wa maendeleo limewezesha wananchi kuishi kwa utulivu na kufanya shughuli zao bila hofu.
Kupitia amani hii, Watanzania wameweza kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa uhuru mkubwa. Michezo, biashara, elimu na ibada vimekuwa vikifanyika kwa utulivu mkubwa,vilevile Vijana wamepata nafasi ya kusoma na kujiendeleza, huku watu wa dini mbalimbali wakifanya ibada zao kwa uhuru.
Haya yote ni matokeo ya juhudi za waasisi wa taifa letu ambao waliweka msingi wa umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania.
Mch.Mwaisaka anasema Amani ikikosekana hali hiyo huleta hofu kwa wananchi na kuhatarisha maendeleo katika sekta mbalimbali kama vile elimu, uchumi na hata uhuru wa kuabudu hivyo Ni muhimu kutambua kuwa amani si jambo la kudumu bila jitihada, bali inahitaji kulindwa na kila mmoja wetu kwa nguvu zote.
Katika mazungumzo mbalimbali ya kijamii, ndugu Hendry Lema, ambaye ni mzee mstaafu wa kanisa la KKKT Usharika wa Engarenaro Arusha, amekuwa akisisitiza umuhimu wa amani kwa maendeleo ya taifa. Anasema kuwa amani ndiyo nguzo kuu inayowezesha jamii kustawi, na bila amani hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana.
"Mimi ni baba na Kichwa cha familia pia ni mlezi wa kiroho na mshauri wa jamii, nahimiza watu kurejea katika misingi ya upendo, heshima na kuvumiliana,
Ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa tunadumisha misingi hii ya upendo na mshikamano. Kama alivyotuasa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, upendo ni silaha kubwa inayoweza kuondoa chuki, ubaguzi na migogoro.
Tukizingatia hilo, tutaweza kujenga taifa lenye umoja na lenye kuheshimiana kati ya wananchi na viongozi wao, tutangulize utu ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.
Mwisho, nitoe wito kwa Watanzania wote bila kujali dini au imani zao, kuendelea kuliombea taifa letu na kumtanguliza Mungu katika kila jambo. Tukiwa na moyo wa toba na unyenyekevu,
Mungu atatusaidia kulinda amani yetu na kutujalia haki ya kweli. Kama ilivyoandikwa katika Mithali 14:34, “Haki huinua taifa; bali dhambi ni aibu ya watu wote.” Mungu ibariki Tanzania, Mungu tubariki Watanzania.
BENY Israel Mwaisaka, mchungaji wa kanisa la FPCT Komwale lililopo nje kidogo ya mji wa Handeni mkoani Tanga


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...