Jumla ya washiriki 37 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda(UCAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia(SCAA) na nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea (Conakry), ambazo zinajumuishwa katika Roberts Flight Information Region (Roberts FIR), wamehitimu mafunzo kozi nne tofauti yaliyolenga kuimarisha usalama na ufanisi wa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika katika Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Salim Msangi, amefunga rasmi kozi hizo za Usimamizi wa Uongozaji Ndege katika hafla iliyofanyika Aprili 2, 2026 katika Makao Makuu ya TCAA, Ukonga–Banana, Dar es Salaam.
Akizungumza, katika hafla hiyo Bw. Msangi aliwapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na mafanikio waliyoonesha, na kutoa shukrani kwa mamlaka za anga za Somalia, Uganda, na Robert FIR kwa kushirikiana na CATC katika kuendeleza taaluma ya usafiri wa anga.
Bw. Msangi alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwa kitovu cha mafunzo ya usafiri wa anga barani Afrika kutokana na uwekezaji katika miundombinu ya mafunzo na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Bw. Msangi pia aliwahimiza wahitimu kufuata taratibu za usalama, kufanya kazi kwa umakini, kudumisha mawasiliano sahihi, na kuweka usalama mbele katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha CATC, Bw. Aristid Kanje, alisema kuwa mafunzo haya yamejwajengea washiriki uwezo wa kitaaluma kwa wahitimu na kuwawezesha kutoa huduma ya udhibiti wa anga kwa usalama, kwa ufanisi na kwa weledi.
Mchanganuo wa kozi zilizohitimishwa ni pamoja na kozi ya ‘Basic Aerodrome Control’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 13 Oktoba hadi 21 Novemba 2025; kozi ya ‘Aerodrome Control’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 24 Novemba 2025 hadi 30 Januari 2026; kozi ya ‘Area Control Procedural’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 2 Februari hadi 3 Aprili 2026; pamoja na kozi ya ‘Basic Aerodrome’, iliyohusisha washiriki 16 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda (UCAA) na Roberts FIR, iliyoanza tarehe 23 Februari hadi 3 Aprili 2026.
Aidha, Bw. Ahemed Moulin Hasson kutoka SCAA alitoa shukrani na kuhimiza mshikamano kati ya mamlaka za anga za Afrika na CATC, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuimarisha usalama na ufanisi wa anga.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi akizungumza na wahitimu wa kozi mbalimbali wakati wa kufunga kozi hizo zilizokuwa zinatolewa na CATC.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Somalia (SCAA) Ahemed Moulin Hasson akizungumza namna Mamlaka hiyo inavyotoa nafasi kwa watumishi wao kusoma kozi mbalimbali.

Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), Aristid Kanje akizungumza kuhusu Chuo hicho kilivyoweza kutoa mafunzo ambayo yamewajengea uwezo wa kitaaluma kwa wahitimu ili kuwawezesha kutoa huduma ya udhibiti wa anga kwa usalama, kwa ufanisi na kwa weledi.










Baadhi ya wahitimu, walimu pamoja na watumishi kutoka CATC, SCAA na TCAA wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi alipokuwa anafunga kozi hizo.





Mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi pamoja Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Somalia (SCAA) Ahemed Moulin Hasson wakikabidhi vyeti kwa wahitimu.



Mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi pamoja Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Somalia (SCAA) Ahemed Moulin Hasson wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu, Baadhi ya Menejimenti ya TCAA na walimu wa CATC wakati wa kufunga kozi hizo


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...