-Asema kuna miradi inakwama utekelezaji sababu ya migawanyiko

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waepuke migogoro na mizozo kwa sababu kuna miradi inakwama utekelezaji kutokana na migawanyiko.

“Twendeni tukatimize wajibu wetu, tuache migawanyiko kwa sababu hayo si matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza wakati akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.

Ametoa wito huo leo jioni (Jumatano, Aprili 22, 2026) wakati akifungua mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo na kusisitiza kuwa waangalie uwezekano wa kuondoa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti ambao hivi sasa unafanyika kila mwaka.

“Tuepuke migogoro, Waheshimiwa Mameya, Madiwani na Wenyeviti; kuna baadhi ya maeneo tunachelewa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu ya migogoro inayotengeneza migawanyiko.”

“Ondoeni utaratibu wa kuchagua Makamu Mweneyekiti kila mwaka kwani jambo hili linaleta makovu. Nimeshamuagiza Waziri wa TAMISEMI amuandikie Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ni sheria ifutwe, kama ni kanuni ibadilishwe, lakini kama mkutano huu una mamlaka, utaratibu wa kuchagua Makamu Mwenyekiti kila mwaka ufutwe,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema utaratibu wa sasa unawanyima fursa viongozi walioko madarakani kujielekeza kwenye masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi na badala yake wanajikuta kwenye harakati za kugawana vyeo.

“Wenyeviti wanajikuta wanaongoza watu waliogawanyika na hili halileti tija. Hivi sasa walioko madarakani bado wanajifunza kazi, tayari wengine wameshaanza kampeni kuwania nafasi zao,” amesisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi watakaochaguliwa kesho wahakikishe wanakuwa chachu ya maendeleo na kusimamia maslahi ya wananchi kwa vitendo na kuongeza: “Kwa viongozi mtakaochaguliwa, mhakikishe mnakwenda kusaidia Jumuiya yetu na maslahi ya wananchi, muwe viongozi wanaopinga rushwa kwa vitendo. Mhakikishe mnakuwa daraja la kuleta maendeleo kwa wananchi na kuitafsiri Dira ya 2050.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa 2050, akiwataka viongozi wa Halmashauri wawe wasimamizi na walezi wa mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Katika DIRA 20250, sekta binafsi imepewa asilimia 70 za kutoa mchango. Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri mkawe walezi wa sekta binafsi. Mkitanguliza kulea sekta binafsi mtakuza mapato. Mkitanguliza mapato mtaua sekta binafsi. Sekta binafsi tunaitegemea sana katika kutengeneza ajira kwa akinamama na vijana,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi hao kutojihisi dhaifu katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wao mkubwa licha ya changamoto chache zinazojitokeza.

“Msipate unyonge, Mheshimiwa Rais anatambua kazi kubwa ya usimamizi wa miradi ya maendeleo mnayoifanya; ni kweli kuna baadhi ya wachache wanaotuangusha, lakini wengi wenu mnafanya kazi vizuri sana,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwahakikishia wajumbe wa mkutano kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala la kuboresha maslahi ya madiwani kama ambavyo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa ALAT anayemaliza muda wake, Bw. Murshid Ngeze.

“Niwahakikishie Mheshimiwa Rais anatambua kazi kubwa madiwani mnayoifanya; jambo lenu linajitosheleza na linaeleweka, Serikali inaendelea kulifanyia kazi,” amesema.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...