Mratibu wa Wanawake kwenye Sekta ya Gesi ya LPG kutoka Chama cha Wadau wa Gesi Tanzania TZLPGA Winner Joram Lukumay, amesema tafiti zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanaotumia gesi ya LPG kupikia ni wanawake.
Hali inayodhihirisha nafasi kubwa ya wanawake katika mapinduzi ya matumizi ya nishati safi nchini pamoja na mchango wao katika kulinda afya na mazingira.
Akizungumza wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Taasis hiyo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Mei 22, 2026 Jijini Dodoma , amewahamasisha vijana hususani wanawake kujitokeza kwa wingi kusoma taaluma zinazohusiana na sekta ya gesi.
Lukumay amesema licha ya wanawake kuwa watumiaji wakubwa wa nishati safi ya kupikia, bado idadi yao katika taaluma na ajira ndani ya sekta ya mafuta na gesi ni ndogo ukilinganisha na wanaume.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wanafunzi maarifa na kuwaandaa kwa ajira pamoja na fursa za biashara katika sekta ya LPG ambayo inaendelea kukua nchini, huku akiwataka wanawake kujiamini na kupambana kuhakikisha wanapata uwiano sawa katika taaluma hiyo.
Aidha, amesema Serikali chini ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo matumizi ya gesi ya LPG kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo wa chakula maarufu kama mamalishe ili kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.
Kwa upande wake, Afisa wa Ufundi wa TZLPGA, Mhandisi Huruma Msigwa amesema elimu kuhusu matumizi salama ya gesi bado inahitajika kwa wananchi wengi ili kuondoa ajali za gesi ambazo mara nyingi husababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.
Akitoa rai kwa jamii kuacha mila potofu ya kusema chakula kinachopikwa na gesi sio kitamu kama cha kupika kwenye mkaa, kwani tafiti zimefanyika na kubaini kuwa hakuna uhalisia wowote.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wamesema yamewapa uelewa mkubwa kuhusu sekta ya LPG pamoja na fursa zilizopo, huku wakieleza kuwa yamewaongezea hamasa ya kujikita zaidi katika taaluma na shughuli zinazohusiana na nishati safi ya kupikia, pamoja kuhakikisha wanakuwa chachu kwa kuipeleka elimu hiyo kwa jamii.
Katika mafunzo hayo zaidi ya wanafunzi 120 kutoka kada mbalimbali ikiwemo Shahada ya Science in Petroleum Engineering, Chemical and Processing Engineering, Mineral Processing Engineering pamoja na taaluma za Earth Sciences and Engineering kutoka College of Earth Sciences and Engineering (COESE) wamenufaika na mafunzo hayo.
Mafunzo hayo pia yamelenga kuunganisha maarifa ya darasani na mahitaji ya sekta ya mafuta na gesi kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu, wafanyabiashara na mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...